Lwanga azua utata usajili wa Msimbazi

Dar es Salaam. Gumzo kubwa kwa sasa ni utata wa usajili wa kiungo mganda, Thadeo Lwanga, ambaye jina lake halionekani kwenye usajili wa Simba uliotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Jana, TFF ilitoa orodha ya majina ya wachezaji wote waliosajiliwa katika dirisha dogo na klabu mbalilimbali zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la

Kwanza na Ligi ya Wanawake Bara, lakini jina la Lwanga halikuwemo kwenye usajili wa Simba.

Katika usajili wa Simba kwenye dirisha dogo yameonekana majina mawili tu ya wachezaji wa kimataifa ambao ni Perfect Chikwendwe waliosajili kutoka FC Platinum ya Zimbabwe na mcongo Doxa Gikanji ambaye anatokea klabu ya DC Motema Pembe ya Congo.

Kutoonekana kwa Lwanga ambaye alitambulishwa na Simba Desemba 12 mwaka jana, baada ya kusajiliwa na na alicheza kwa kiwango kikubwa kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi yaliyomalizika Janauri 13.

Swali kutoka kwa wadau wengi ni kwa nini jina la mchezaji huyo halijaonekana kwenye usajili wa Simba uliotumwa TFF au amesajiliwa ili kutumika kwa mashindano ya kimataifa tu?.

Simba hivi sasa imetimiza idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni, hivyo kushindwa kuendana na sheria za Ligi Kuu Bara, ambazo zinataka wachezaji wa kigeni wasiozidi 10 hivyo kama timu hiyo itazidi idadi hiyo itabidi baadhi ya wachezaji wacheze mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pekee.

Licha ya gazeti hili kufanuyajitihada za kuwatafuta viongozi wa Simba kutoa ufafanuzi wa jambo hilo, lakini simu zao ziliita bila kupokelewa.

Kwa upande wake, Lwanga, ambaye alikiri kuwa amesajiliwa na Simba kwa mkataba ambao unamtaka kucheza ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa.

“Mimi ni mchezaji wa Simba na ambaye nilisajiliwa kama mchezaji huru kaba ya dirisha dogo kufunguliwa na usajili wangu unaonyesha kuwa nitacheza mashindano ya ndani na kimataifa.

“Nilikatiwa tiketi ya kwenda likizo Uganda na Jumapili ndiyo narudi tayari kuendelea kutimiza majukumu yangu katika timu yangu mpya,” alisema Lwanga

Mkurugenzi wa Sheria Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura alisema usajili uliowasilishwa TFF kwa klabu zote ndiyo huo waliouweka wazi.

“Huo tulioutoa ndiyo usajili wa klabu zote kwenye dirisha dogo, sasa kama kuna jina halipo waulizwe klabu husika. Hivi sasa ni kipindi cha mapingamizi, hivyo mwenye pingamizi lolote kwa mchezaji aliyepo hapo anatakiwa kuwasilisha TFF,” alisema Wambura.