Lwanga aanza Simba ikiivaa Tanzania Prisons

KIUNGO mkabaji Taddeo Lwanga ameanza kwenye kikosi cha kwanza kilichopangwa leo kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.

Lwanga anarejea baada ya kupona majeraha wiki chache zilizopita ambapo mara kadhaa amekuwa akiingia kutokea benchi lakini kwenye mchezo huu Kaimu Kocha Mkuu, Selema Matola amemuongoza ili kuongoza safu ya kiungo.

Kwenye eneo la katikakati nyota huyo atacheza sambamba na Erasto Nyoni huku beki wa kati Joash Onyango akirejea pia baada ya kukosa mechi tatu.

Kwa upande wa ushambuliaji Meddie Kagere ataendelea kuongoza mashambulizi akisaidiwa na viungo washambuliaji Peter Banda, Kibu Denis na Yusuf Mhilu.

Kikosi kamili kinachoanza ni Beno Kakolanya, Jimmyson Mwanuke, Gadiel Michael, Joash Onyango, Kennedy Juma, Taddeo Lwanga, Kibu Denis, Erasto Nyoni, Medie Kagere, Peter Banda na Yusuf Mhilu.

Wachezaji wa Akiba ni Ally Salim, Henock Inonga, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, John Bocco, Hassan Mussa U-20, Shafii Hassan U-20 na Kassim Omary U-20.

Timu hizi zinakutana katika mchezo wa 29, ambapo Tanzania Prisons inashika nafasi ya 15 na pointi 26 huku Simba ikiwa ya pili na pointi 60.