Luis Miquissone azua gumzo Afrika

Wakati taarifa za Luis Miquissone kuhitajiwa na timu mbalimbali barani Afrika zikipamba moto, mshambuliaji huyo wa Simba ameingia katika orodha ya nyota wanne wanaopigiwa kura ya kumchagua mchezaji bora wa wiki wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika orodha hiyo, Miquissone anashindana na nyota wa Mamelodi Sundowns, Themba Zwane, Muaid Ellafi (Wydad Casablanca) na Obed Mayamba Mukokiani wa AS Vita Club.

Miquissone ameingia katika kinyang'anyiro hicho baada ya kuonyesha kiwango bora na kufunga bao pekee la ushindi wa Simba katika mchezo dhidi ya Al Ahly ya Misri uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Jumanne iliyopita.

Wakati Miquissone akifanya hayo upande wa Simba, mshindani wake, Themba Zwane yeye ameingia baada ya kuifungia Mamelodi Sundowns mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-1 walioupata dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, jana Jumapili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwa upande wa Muaid Ellafi wa Wydad Casablanca yeye alitoa mchango mkubwa katika ushindi wa mabao 4-0 ambao timu yake iliupata dhidi ya Kaizer Chief ya Afrika Kusini jana Jumapili ambapo alipiga pasi moja iliyozaa bao wakati Mayamba Mukokiani  aliifungia AS Vita mabao mawili pindi ilipoibuka na ushindi wa mabao 4-1 ugenini dhidi ya Al Merreikh ya Sudan.

Kura za kumchagua mchezaji bora wa wiki zinapigwa katika ukurasa wa mtandao wa Twitter wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) na mshindi atajulikana kesho mnamo saa 8.00 alasiri.