Luis ashusha presha Simba, aitibulia Prisons kwa Mkapa

Muktasari:

Bao la winga Luis Miquissone katika dakika  ya nne kati ya tano za nyongeza limeilindia aibu Simba wakichomoa bao jioni wakati wakilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prissons mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Bao la winga Luis Miquissone katika dakika  ya nne kati ya tano za nyongeza limeilindia aibu Simba wakichomoa bao jioni wakati wakilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prissons mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Sare hiyo Simba hawatamsahau kipa wa Prisons Jeremia Kisubi ambaye alikuwa mwiba kwa wekundu hao kwa kuokoa michomo mingi mikali.

Sare hiyo inaifanya Simba kuambbulia pointi moja wakiwaachia Prisons pointi nne katika mechi mbili msimu huu.

Mchezo ulivyokuwa

Timu zote ziliuanza mchezo kwa mbinu zake wenyeji Simba wakionyesha kutaka kuweka mpira chini kwa kucheza soka lao la pasi nyingi lakini Prisons nao kama kawaida yao wakionyesha wameiva kwa stamina wakitumia nguvu nyingi.

Katika hali ya kuchekesha Prisons ndio walioanzisha mpira wakianza kwa kuutoa nje mara mbili na kuwa wa kurushwa katika nusu ya wenyeji wao.

Wageni hao walifanya hivyo mara mbili hata pale waliporushiwa walirudia kitendo hicho kisha baadaye kuamua kucheza.

Dakika ya 12 Simba walifanya shambulizi zuri shuti la kiungoRally Bwalya linapaa alipokea pasi ya Muzamiru Yassin.

Prisons walijibu shambulizi kama hilo dakoka ya 16 shuti la Jeremia Juma akiwa mbali na eneo la hatari linapanguliwa na kipa Aishi Manula kisha anadaka vyema.

Luis Miquissone alipata nafasi nzuri dakika ya 21 lakini naye shuti lake lilipaa juu la lango.

Dakika ya 24 Prisons walilazimika kumtoa beki wake wa kati Nurdin Chona aliyepata maumivu nafasi yake ikichukuliwa na Dotto Shaban.

Dakika ya 27 Simba walifanikiwa kupata penalti iliyotokana na mwamuzi Emmanuel Mwandembwa kutoka Arusha kudai beki Vedastus Mwihambi ameunawa wakati akitaka kumzuia Chris Mugalu kuuchukua.

Hata hivyo Mugalu aliipiga penalti hiyo kisha kipa Jeremia Kisubi kuupangua na kuwa kona iliyokosa madhara.

Prisons walipata pigo wakitakiwa kucheza pungufu baada ya beki wake Jumanne Elfadhil kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi Mwandembwa baada ya kuonekana kuinua mguu vibaya wakati akikabana na Mzamiru.

Simba walipiga shuti pekee lililolenga lango katika dakika ya pili ya nyongeza kati ya tatu likipigwa na beki wa kulia Shomari Kapombe Kisubi anapangua na kuwa kona.

Mpaka mapumziko timu zote zilimaliza kipindi cha kwanza wakiwa suluhu.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kumtoa Mzamiru wakimuingiza nahodha wao mshambuliaji John Bocco mabadiliko yaliyolenga kuongeza kasi ya kuongeza nguvu ya kutafuta bao.

Dakika ya 56 Prisons walifanikiwa kupata bao la kuongoza likifungwa na beki wa kulia Salum Kimenya kwa shuti la mguu wa kulia.

Bao hilo lilitokana na mpira wa adhabu Kimenya akifunga moja kwa moja nje kidogo ya eneo la hatari baada ya beki wake Joash Onyango kuunawa wakati akiwa kwenye hatakati za kuokoa.

Kuingia kwa bao hilo Simba wakamtoa Perfect Chikwende nafasi yake ikienda kwa Clatous Chama dakika moja baada bao hilo.

Simba walifanya shambulizi kali dakika ya 60 shuti la Miquissone linaokolewa na nahodha ww Prisons Benjamin Asukile karibu na mstari wa goli kwa kichwa.

Simba waliendelea kuliandama lango la Prisons dakika ya 64 Mugalu anapachika bao wavuni akimalizia mpira uliotemwa na Kisubi kufuatia shuti la beki Mohammed Hussein 'Tshabalala lakini tayari kibendera cha msaidizi wa mwamuzi namba mbili Abdulaziz nilikuwa juu akidai mfungaji alikuwa ameotea wakati shuti hilo linapigwa.

Dakika ya 67 Simba wakafanya mabadiliko ya mwisho wakimtoa Bwalya nafasi yake ilichukuliwa na Bernard Morrison.

Tangu Prisons wapate bao walizidi kucheza kwa kujilinda zaidi huku  wakishambulia kwa kushtukiza

Dakika ya 73 Prisons walimtoa mshambuliaji Samson Baraka nafasi yake ikachukuliwa na mwenzio Kassim Mdoe wakiongeza nguvu ya eneo lao la ushambuliaji.

Dakika mbili baadaye Kisubi anafanya kazi ya dhahabu kwa timu yake akipangua shuti kali la Kapombe akiunasa mpira uliokolewa na mabeki wa Prisons na kuwa kona ambayo nayo ilitengeneza nafasi nzuri kwa Simba lakini kichwa cha Bocco kinadakwa vizuri na kipa huyo tena.

Dakika ya 85 Simba wanatengeneza mashambulizi mawili mazuri akitangulia Chama anawachambua mabeki wa Prison lakini wakati akitaka kufunga lakini Shabam anatokea na kutibua kisha mpira unarushwa krosi ya Tshabalala inatua kichwani kwa Mugalu kinapaa.

Dakika ya 86 Chama anaunasa mpira eneo zuri anaachia shuti kali Kisubi anakaa vyema na kuudaka.

Dakika moja baadaye Simba waliendelea kuhamia lango la Prisons shuti kali la Morrison linapanguliwa na Kisubi ambaye Simba watamkumbuka kwa alivyokuwa mwiba kupatikana kwa bao lao.

Simba bado waliendelea kuganda lango la Prisons wakitengeneza shambulizi lingime dakika ya 88 Pascal Wawa anapaisha akiwa katika eneo zuri kufunga.

Nafasi ya dhahabu kwa simba ilikuwa katika dakika ya pili kati ya tano za nyongeza Mugalu akipaisha akiwa uso kwa uso na Kisubi akipokea pasi ya Chama.

Dakika ya nne kati ya tano za nyongeza Miquissone akaisawazishia Simba kwa kichwa akipokea krosi ya Kapombe.