Kwa mziki huu patachimbika, Sakho, Makambo vita nzito

USAJILI wa nyota wanne uliofanywa na Yanga katika dirisha dogo la usajili litakalofungwa Januari 15, umeipa timu hiyo vikosi viwili vikali ambavyo kila kimoja kinaweza kucheza mechi yaoyote ngumu ikiwa ya watani bila presha yoyote.

Kabla ya kuongeza nyota hao, Yanga haikuwa na kikosi imara cha pili ambacho kingeweza kupambana na Simba na kutoa upinzani mkubwa au hata kupata matokeo mazuri.

Waliongezwa na kutanua upana wa kikosi cha Yanga ni; kipa Abuutwalib Mshery, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na washambuliaji Denis Nkane na Crispin Ngushi.

Kwa sasa Yanga ina uhakika wa idadi kubwa ya wachezaji wa benchi wanaoweza kuingia kuwasha moto ule yule wa wenzao watakaoanza tofauti na mwanzoni.

Licha ya kuwa na kikosi imara cha kwanza, kabla ya dirisha dogo, Yanga haikuwa na kikosi imara cha wachezaji wa akiba ambao wangeweza kuwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo pale wale wa kikosi cha kwa wa kikosekana tofauti na ilivyo kwa Simba.

Licha ya Simba kutosajili yeyote katika dirisha hilo hadi sasa, timu waliyonayo inaunda vikosi viwili vya ushindani na huenda Yanga imegundua hilo na kuamua kuingia sokoni kwa nguvu kipindi hiki na kuonekana kuwapa kile ilichowapa kiburi Wekundu wa Msimbazi.

Kama ilivyo kwa Simba ambayo upana wa kikosi chake hauwapi hofu kukutana na watani wao, hata ikiwakosa baadhi ya nyota muhimu, ndivyo ilivyo kwa Yanga kwa sasa kutokana na usajili walioufanya na ubora wa wachezaji waliowaongeza kwa kuunganisha na wale waliopo kikosini.

Wakati vikosi viwili vya Simba vikionekana vinaweza kucheza kwa mifumo tofauti ya 4-2-3-1 na 4-4-2 bila presha kwa Yanga nako sasa chao cha kwanza kinaweza kumudu vyema mfumo wa 4-2-3-1 inayoupendelea na kusiwe na tofauti kubwa na kile cha pili kikicheza 4-4-2.

Katika mfumo wa 4-2-3-1 kikosi cha kwanza cha Simba kinachoweza kupambana na Yanga ni kile kilichozoeleka cha kipa Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Henock Inonga, Joash Onyango, Jonas Mkude, Pape Osmane Sakho, Sadio Kanoute, Medie Kagere, Rally Bwalya na Bernard Morrison.

Kikosi cha pili kinachoweza kuimudu Yanga bila presha ikitokea nyota wa kikosi cha kwanza hawapo kinaundwa na kipa Beno Kakolanya, Israel Mwenda, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Taddeo Lwanga, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Chris Mugalu, Kibu Denis na Peter Banda.

Wakati huo kutakuwa na wachezaji wengine wa ziada wa wanaoweza kutumika kutoa sapoti wakiwamo Ally Salim, Jimmyson Mwanuke, Erasto Nyoni, John Bocco na Yusuph Mhilu.

Kwa upande wa Yanga, mziki katika kikosi cha kwanza unaundwa na kipa Djigui Diarra, Djuma Shabani, Kibwana Shomary, Dickson Job, Bakar Mwamnyeto, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Khalid Aucho, Fiston Mayele, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Saido Ntibazonkiza.

Kikosi cha pili cha Yanga kinachoweza kuivaa Simba freshi tu bila ya hofu hasa kikitumia mfumo wa 4-4-2, kinaundwa na kipa Abuutwalib Mshery, Paul Godfrey, Yassin Mustafa, Abdallah Shaibu, Mukoko Tomombe, Zawadi Mauya, Denis Nkane, Salum Abubakar, Heritier Makambo, Crispin Ngushi na Dickson Ambundo.

Wachezaji wa ziada kwa upande wa Yanga ni Erick Johora, David Bryson, Mapinduzi Balama, Yusuph Athuman, Deus Kaseke, Farid Musa na Songne Yacouba.

Katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu iliyopigwa Desemba 11, mwaka jana Simba ikiwa wenyeji, timu hizo hazikufungana. Kwa sasa kuna dalili huenda zikakutana katika mechi yao ya kwanza kwa 2022 kupitia fainali za Kombe la Mapinduzi inayoelekea ukingoni.

Timu hizo zimetinga nusu fainali, Yanga ikitarajiwa kucheza na Azam, huku Simba ikijiandaa kuwavaa Namungo. Iwapo zote zitachanga vyema karata zao kesho, ni wazi zitakutana kwa mara ya pili mfululizo katika mechi ya fainali ya Mapinduzi.

Msimu uliopita katika michuano hiyo, Yanga iliizima Simba kwa mikwaju ya penalti 4-3. baada ya dakika 90 kuisha bila bao. Kitu cha kuvutia ni kwamba ilivyokuwa nusu fainali zilizopita kila timu ilikutana na mpinzani wake wa msimu huu. 2021 Simba iliing’oa Namungo na Yanga kuiondosha Azam katika nusu fainali.


WASIKIE WADAU

Kocha wa zamani wa Biashara United, Amani Josiah alisema licha ya Simba kutofanya usajili wowote hadi sasa, hadhani kama inapaswa kutishika na usajili wa Yanga.

“Yanga ipo katika kiwango cha juu sana, ila nikiangalia wachezaji iliowasajili sioni wa kuwatoa wale waliopo kikosi cha kwanza. Kwani wale wanaoanza kwa sasa wako katika kiwango cha juu sana labda ilete wengine,” alisema Josiah na kuongeza;

“Simba iko vizuri na ukiangalia pengo la pointi haliko mbali, shida watu wanaihukumu kwa kuangalia kikosi cha Yanga. Simba inapata matokeo, huku ikiwa haijaimarika wakati Yanga inapata matokeo huku ikiwa imeimarika. Jambo la msingi ni kusubiri kuona. Kama ni ushauri, nadhani Yanga inapaswa kusajili watu wenye uwezo wa kuwatoa wanaoanza kikosini.”

Naye straika wa zamani wa Azam na Kagera Sugar, Phillip Alando alisema ubora wa kikosi au usajili hautoshi kuamua matokeo ya mechi ya watani, kwani ni historia ya mechi za vigogo zilivyo,” alisema Alando na kuongeza;

“Yanga wameimarisha kikosi kwa kupanua kikosi, hivyo itatoa nafasi kwa wachezaji tofauti tofauti vya kutosha iwe katika ligi na Kombe la Shirikisho ASFC. Wachezaji wameimarika na wanacheza kwa kuelewana sana na zaidi ya yote ni uwepo wa nyota wenye uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja.”

Alando pia alisema; Ukimya wa Simba sio tatizo. Soka ni mabao na bado ninawaona wale watu watatu walioongoza kwa mabao msimu uliopita bado wapo ndani ya kikosi, yaani Bocco (John), Mugalu (Chris) na Medie Kagere. Wanaonekana wanayumba, ila Simba ina timu imara. Pale nyuma haijamuondoa mtu zaidi kumuongeza Henock.”

“Endapo atatokea mchezaji mmoja au wawili wakafikia ubora hasa kwa hawa wageni basi, Simba itabaki kuwa ile ile. Kama zitakutana wenyewe (Simba na Yanga)sina turufu ya timu ipi itashinda, kwani mechi hii huwa inatekwa na maneno mengi kuliko ufanisi wa uwanjani,” alisisitiza Alando.


VITA NZITO

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Heritier Makambo pamoja na Pape Ousmane Sakho na Reliants Lusajo wa Namungo watakuwa na vita yao ya kuwania tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya Mapinduzi, wakati timu zao zitakapoumana kwenye mechi za nusu fainali zinazochezwa kesho.

Azam itavaana na Yanga saa 10 jioni na Simba na Namungo kumalizana saa 2 usiku - mechi zikipigwa Uwanja wa Amaan, huku nyota wa timu hizo watakuwa wakiwania kutupia ili kuzipeleka timu zao fainali na pia kubeba tuzo ya mfungaji bora.

Msimu uliopita tuzo hiyo ilibebwa na Miraji Athuman aliyekuwa Simba akifunga mabao manne, huku Francis Kahata pia aliyekuwa Simba alikuwa Mchezaji Bora na kipa Faruk Shikhalo aliyekuwa Yanga alitwaa ile ya Kipa Bora. Wachezaji hao wote hawapo kwenye michuano ya msimu huu.

Makambo ndiye kinara wa sasa akiwa na mawili, sawa na Abrahman Ali wa KMKM na Hussein Mwinyi wa Meli 4 City ambazo timu zao zimeshaaga michuano hiyo.

Sakho na Rally Bwalya wa Simba wana bao moja moja kama ilivyo kwa Lusajo, Obrey Chirwa, Sixtus Sabilo wote wa Namungo, Idd Chilunda na Kenneth Muguna wa Azam ambao kama watazitumia vyema mechi za kesho wanaweza kujitengenezea nafasi ya kubeba tuzo hiyo.

Wengine wenye bao moja moja kwenye timu hizo ni Denis Nkane na Feisal Salum wote wa Yanga kama wakikomaa kesho wanaweza utamu wa vita hiyo ya mfungaji bora inayoendana na mkwanja wa maana kutoka kwa waandaaji na wadhamini wa michuano hiyo.

Fainali za michuano hii itapigwa Januari 13 na kuhitimishwa msimu wa 16 wa michuano hiyo iliyoasisiwa kwa mfumo wa sasa tangu mwaka 2007, huku Azam ikiwa imetwaa ubingwa mara tano ikifuatiwa na Simba iliyobeba mara tatu na kufuatiwa na Yanga yenye mbili kama Mtibwa Sugar. Yanga kwa sasa ndio watetezi wakilitwaa msimu uliopita wakiifunga Simba kwa penalti.