Kwa mfumo huu wameumia

UTAMU wa pambano la watani wa jadi kati ya Simba na Yanga unazidi kupanda baada ya kuwepo tambo nyingi huko mtaani kutoka kwa mashabiki wa timu hizo kongwe nchini.

Muda mfupi ukiwa umebaki kabla ya mechi hiyo, kikosi cha Yanga msimu huu kimebadilisha makocha wanne ambao kila mmoja alikuwa na mfumo wake.

Yanga walianza na Zlatko Krimpotic akafuata Cedrick Kaze aliyeongoza mechi mbili dhidi ya Simba kwenye ligi mzunguko wa kwanza na fainali ya Mapinduzi.

Baada ya hapo akafuata Juma Mwambusi ambaye amemuachia Nabi Mohamed atakayeiongoza Jumamosi.

Kutokana na ingia toka ya makocha hao Yanga, ni mfumo upi wanatakiwa kuutumia ili kuvuna pointi tatu dhidi ya Simba ambao ukweli usiopingika wapo imara na bora katika kushambulia?

Mfumo wa kwanza unaweza ukawa na faida upande wao ni (4-4-2), aliokuwa anapenda zaidi kutumia Krimpotic.

Faida ya mfumo huu ambao mashabiki wa Yanga hawakuwa wanaupenda, mzuri kwenye kukaba na kulinda Simba ambavyo wapo bora katika kushambulia watawahimili.

Katika mfumo huu Yanga wanakuwa na wachezaji nane mpaka tisa wakizuia mashambulizi ya Simba yanayotokea kwa mabeki wao wa pembeni, Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Wakati huohuo Simba wapo bora kwenye kuanzisha mashambulizi katika eneo la kiungo wanapocheza mara kwa mara Clatous Chama, Luis Miquissone, Rarry Bwalya na Bernard Morrison na muda mwingine hufunga wenyewe.

Ukiachana na faida ya kuzuia watakuwa na nyingine kwenye kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo watakuwa wanapiga pasi chache kufika langoni mwa Simba. Kutokana na mabeki wa pembeni wa Simba kushambulizia zaidi, pasi inaweza kutoka kwa beki Abdallah Shaibu au mwingine kwenda kwa Tuisila Kisinda na kuwakimbiza wachezaji wachache watakao baki nyuma na kupiga pasi ya mwisho kwa Yacouba Sogne atakayekuwa na nafasi ya kufunga bao.

Zlatko na mfumo wake huo alicheza mechi tano bila ya kupoteza.

Mfumo wa kocha Kaze (4-2-3-1) utafanana na ambao Simba wataanza nao maana yake timu ambayo itakuwa na wachezaji bora na kutimiza majukumu ya nafasi yake ndio itafanya vizuri.

Kaze alikuwa anatumia mabeki wanne, viungo wakabaji wawili, viungo washambuliaji watatu na straika mmoja na kama wakiutumia watakuwa wakipishana katika kushambuliana.

Kocha wa muda Mwambusi alikuwa haeleweki kuna mechi alitumia (4-4-2 au 4-2-3-1) na yote ililenga kushambulia zaidi kuliko kuzuia.

Mwambusi na mfumo wake wa 4-4-2 alikuwa akitumia mabeki wanne, viungo wanne na washambuliaji wawili. Kocha Nabi anaonekana ni mto wa kushambulia zaidi kuliko kujilinda kwani mfumo wake pendwa ni 4-1-4-1 ambao hutumia mabeki wanne, kiungo mkabaji mmoja, viungo washambuliaji wanne na straika mmoja.

Nabi anaweza kuanza na Carlos Carlinhos, Kisinda, Saido Ntibazonkiza, Yacouba na Ditram Nchimbi na Fiston Abdulrazack.


WASIKIE HAWA

Kocha wa zamani wa Toto Africans, John Tegete alisema Yanga wanatakiwa kuingia katika mechi hiyo na nidhamu ila sio kuiogopa Simba kutokana na mwenendo wao wa matokeo mazuri.

“Kwangu kama Yanga wataingia na mfumo wa kushambulia kama ambao wanatumia Simba 4-2-3-1, watabishana nao na wanaweza kuwazidi na wakawafunga,” alisema Tegete.

Mchezaji wa zamani, Abdul Chilumba alisema linapofika suala la mechi hiyo sio muda wa kuangalia mifumo kuna wakati uwezo wa wachezaji binafsi unakwenda kuamua.