Kocha: Njia ilimvuruga Sulle

Muktasari:

Sulle ndiye mwanariadha mwenye kasi zaidi nchini katika mbio za marathoni (kilomita 42).
 

LICHA ya kutwaa ubingwa kwenye mbio za Kili Marathoni, Agostino Sulle ameongeza dakika moja zaidi kwenye muda wake wa awali, huku kocha wake, Thomas Tlanka akibainisha kuwa ugumu wa njia ndio kikwazo kwa mwanaridha huyo.

Sulle alishinda medali ya dhahabu kwenye mbio hiyo akitumia saa 2:18, akiongeza dakika moja zaidi kwenye muda wake wa awali wa saa 2:17.

Muda huo mwanariadha huyo aliuweka kwenye mbio zilizopita za Toronto Marathoni nchini Canada na kuvunja rekodi ya taifa iliyokuwa ikishikiliwa na Juma Ikangaa.

"Ameongeza dakika moja zaidi, lakini hiyo imechangiwa na ugumu wa njia katika mbio za jana Jumapili," amesema kocha Tlanka.

Kocha huyo amesema tofauti na njia iliyotumika kwenye mbio ya Toronto, ile ya Kili Marathoni ilikuwa na milima kwenye baadhi ya maeneo.

"Ilimsababishia kupunguza kasi, ndiyo sababu amekimbia muda mrefu zaidi kulinganisha na muda wake wa awali," amesema Tlanka na kuongeza kuwa;

"Hata hivyo muda huo sio mbaya sana kwake, hasa kipindi hiki ambacho yuko kwenye mazoezi binafsi kujiandaa na mbio za kufuzu Olimpiki.

Amesema mbio za jana Jumapili ndiyo ilikuwa ya kwanza ya majaribio kwa mwanariadha huyo ambaye licha ya kuongeza muda wake, lakini hajakimbia muda mbaya.

"Ana nafasi ya kufanya vizuri na kufuzu kushiriki Olimpki, huo ndio mpango wake na menejimenti yake na hatuna shaka kwamba atajumuishwa kwenye timu ya taifa ya Olimpiki," amesema.