Kocha Mbrazili atua Simba

Kocha Mbrazili atua Simba

Muktasari:

  • Mwananchi linaweza kuthibitisha kwamba, Kocha mpya wa makipa Simba ni Mbrazili, Milton Nienov. Kocha huyo mwenye miaka 52 aliyewahi kuzifundisha Vasco Dagama (Brazil) na Free State Stars, Golden Arrows na Polokwane za Afrika Kusini, tayari yupo jijini Dar es Salaam akisubiri kutangazwa rasmi kuchukua nafasi ya Mohamed Mwarami.

Dar es Salaam. Mwananchi linaweza kuthibitisha kwamba, Kocha mpya wa makipa Simba ni Mbrazili, Milton Nienov. Kocha huyo mwenye miaka 52 aliyewahi kuzifundisha Vasco Dagama (Brazil) na Free State Stars, Golden Arrows na Polokwane za Afrika Kusini, tayari yupo jijini Dar es Salaam akisubiri kutangazwa rasmi kuchukua nafasi ya Mohamed Mwarami.

Mwananchi lilimshuhudia Milton akibarizi kwenye hoteli moja maarufu ya ufukweni jijini Dar es Salaam jana usiku na mmoja na viongozi wa Simba, ambaye alikiri kuwa ni bosi mpya wa makipa lakini atatangazwa kwa utaratibu wa klabu muda wowote.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema kwamba, kocha mkuu na mMsaidizi wake mmoja watakamilisha mambo yao ya kimkataba leo na muda wowote anaweza kutambulishwa kuchukua nafasi ya Sven Vandebroeck aliyetimkia Morocco. Simba chini ya jopo jipya la ufundi, itaanza mazoezi kesho na Jumatano itacheza na Al Hilal ya Sudan kwenye Uwanja wa Mkapa saa 11 jioni katika mechi ya kwanza ya mashindano mapya ya Simba Inter Cup.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez aliwaambia waandishi wa habari jana, mashindano hayo yatahusisha timu tatu, Simba, Mazembe na Al Hilal ya Sudan.

Al Hilal itakwaana na Mazembe Ijumaa kabla ya Simba kufunga na Mazembe Jumapili jioni. Barbara alisema lengo la mashindano hayo ni kuiandaa Simba kimataifa.