Kocha Gwambina atua Mtibwa Sugar, kuanza kazi leo

Muktasari:

  • Kuhusu mkataba wake ndani ya Mtibwa Sugar, amesema baada ya msimu huu kumalizika ndio watakaa meza moja na mabosi wake kujadiliana.

Mwanza. Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Gwambina, Mohamed Badru amethibitisha kutua Mtibwa Sugar na leo Jumapili Mei 16, 2021 ataanza rasmi kibarua chake huku akibainisha kuwa yeye kazi yake ni mpira na changamoto ni sehemu ya kazi.

Badru ambaye alitua Gwambina katikati ya msimu huu akichukua mikoba ya mtangulizi wake, Novatus Fulgence ambaye alifurumushwa na benchi lake akiwamo Msaidizi wake Athuman Bilali 'Billo'.

Akizungumza na Mwanaspoti leo Jumapili, Badru amesema tayari ameshawasili kikosini humo tangu jana jioni na leo atamalizia taratibu zote kisha kuanza majukumu jioni kuitumikia Mtibwa Sugar.

Amesema anafahamu mazingira waliyopo Mtibwa Sugar lakini yeye kama Kocha mwenye taaluma hawezi kukwepa changamoto yoyote bali hali hiyo ndio inamfanya kudhihirisha utaalamu wake.

"Kuhusu Gwambina nitabaki nao kimahusiano kwa sababu ndio wamenitamburisha kwenye soka la Tanzania, ila walisahau kunipa mkataba wa kueleweka kwani kwa muda wote ni kama sikuwa na kandarasi kwahiyo nimepata sehemu mpya yenye maslahi mazuri na leo nitaanza program" amesema Badru.

Kocha huyo Mzanzibar, ameisimamia  Gwambina michezo 10, akishinda minne, sare moja na kupoteza mitano na kuiacha nafasi ya 15 kwa pointi 30 kwenye msimamo wa Ligi, huku akitua Mtibwa Sugar iliyopo nafasi ya 17 hivyo kumpa wakati mgumu kuinusuru timu hiyo  iliyoondokewa mapema na aliyekuwa Kocha wake, Zuberi Katwila