KMC, Biashara vita yapamba moto

VITA ya kuiwania nafasi ya nne ndani ya Ligi Kuu Bara imeendelea kupamba moto na timu zinazoonekana kumenyana zaidi ni KMC na Biashara United Mara.

Timu hizo leo zimekutana kwenye muendelezo wa Ligi Kuu katika mchezo ulioanza saa 8:00 mchana katika dimba la Uhuru, Jijini Dar na kipindi cha kwanza kimemalizika kwa Biashara kuongoza bao 1-0.

Biashara ilijipatia bao la hilo dakika ya 45 kupitia kwa mshambuliaji wake Christian Zigah ambaye aliupiga mpira uliokuwa umemgonga mchezaji wa KMC baada ya Abdul Majid Mangalo kupiga shuti.

Bao hilo la Zigah linakuwa la tano kwake kuifungia Biashara kwenye Ligi Kuu kwa msimu huu ambapo ameonekana kuwa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo.

Dakika ya 48, baada ya KMC kuchonga kona mchezaji wa Biashara alishika kwenye boksi na mwamuzi Omary Mdoe akaamuru penalti ipigwe kuelekezwa Biashara na Emmanuel Mvuyekure alienda kupiga na kusawazisha.

Baada ya KMC kusawazisha, Biashara ilionekana kupania ili kuhakikisha inaibuka na ushindi kwenye mechi hiyo.

Juhudi hizo ziliambatana na kuzidisha mashambulizi kwenda lango la KMC na dakika ya 63 beki wa KMC akaushika mpira kwenye eneo la boksi na mwamuzi akaizawadia Biashara pigo la penalti.

Pigo hilo halikuwa na manufaa yoyote kwani mpigaji Deogratius Judika Mafie alishindwa kupiga kwa ufanisi na golikipa wa KMC, Juma Kaseja alifanikiwa kuudaka mpira kiulaini.


Sare hiyo imeendelea kuifanya vita ya kugombania nafasi ya nne baina ya timu hizo kuzidi kupamba moto.

Biashara inashika nafasi ya nne ikiwa na alama 41 baada ya kucheza mechi 27, wakati KMC inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 40 nayo pia ikicheza mechi 27.