KIU yanusurika kushuka daraja kwenye kikapu

Timu ya KIU imenusurika kushuka daraja kwenye Ligi ndogo ya RBA (RBA Division One).

Baada ya Ligi hiyo kumalizika karibuni, timu ya AFC ilishuka daraja sanjari na Patriot iliyokuwa na pointi tano huku Kigamboni na KIU ambazo zilikuwa mkiani zikifungana pointi.

Timu hizo zilipaswa kutafuta moja itakayoungana na AFC na Patriot kushuka daraja.

"Tulikaa na kujadili ni vigezo gani vitumike kupata timu moja itakayoshuka sanjari na AFC na Patriot.

"Tuliangalia matokeo ya timu hizo kwa mechi zote 20 ilizocheza na KIU kunusurika kwa idadi ya pointi za kufunga na kufungwa," alisema Haleluyan Kavalambi, Mkurugenzi wa ufundi wa Chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam.

Katika Ligi hiyo, KIU na Kigamboni kila moja ilicheza mechi 20 na kufungwa 15.

KIU Ilifunga pointi 1099 na kufungwa pointi 1361 wakati Kigamboni ilifunga pointi 954 na kufungwa 1276 katika mechi zote 20.

Timu hizo kila moja ilishinda mechi tano na kuwa kwenye mstari wa hatari kushuka daraja kabla ya KIU kupenya kwa tofauti ya pointi za kufunga na kufungwa baada ya uamuzi wa kuangalia matokeo ya mechi zao zote za msimu huu.