Kisiga atoa ya moyoni

Muktasari:

Kiungo mkongwe wa Ruvu Shooting, Shaban Kisiga anaamini kama kutakuwa na mifumo mizuri ya kuona vipaji nje ya Simba, Yanga na Azam, timu za Taifa zitakuwa na vikosi vyenye ushindani mkubwa.


KIUNGO wa Ruvu Shooting, Shaban Kisiga amesema kwa namna Tanzania ilivyo na vipaji vikubwa vya soka, kama kungekuwa na mpango maalumu wa kuvitumia ipasavyo basi nchi hii isingekamatika kisoka.

Amesema kwa mifumo iliyopo ni ngumu mchezaji nje ya Simba na Yanga kuonekana
anafanya kitu kikubwa kwa sababu wachezaji wa timu hizo pekee ndio wanatazamwa sana kuliko wengine.
 
"Tanzania kuna vipaji vikubwa, shida inakuja kwenye mifumo. Mfano wachezaji kutoka timu nje ya Simba, Yanga na Azam inakuwa ngumu kutazamwa kama wanavyotazamwa wa hizo klabu, hilo nalo linachangia vipaji vingine visionekane,".  

"Ukiachana na hilo nimewahi kusema kuna vipaji vikubwa kwenye timu za chini huko, kwasababu havitaki kupelekeshwa na watawala ambao hawaujui mpira, wanaona bora wakacheze sehemu ambako wataheshimika,"amesema Kisiga.

Amesema kuna haja yakuona umuhimu wa kuvifuatilia vipaji kwa ngazi ya ligi zote hapa nchini, ili kutengeneza mazingira ya timu ya taifa kuwa na wachezaji wenye uwezo tofauti.

"Naamini kama kungekuwa na ufuatiliaji mzuri hata timu zetu za taifa kwa maana ya wakubwa na vijana zingekuwa na ushindani wa hali ya juu na sio mmoja akiumia basi inakuwa presha kubwa,wakati Tanzania ina vipaji vingi,"amesema.

BY OLIPA ASSA