Kishindo cha Chan, wenyeji wakifungua na Zimbabwe

Dar es Salaam. Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) yanaanza leo Januari 16, 2020 nchini Cameroon kwa wenyeji kuanza kusaka ubingwa dhidi ya Zimbabwe.

Mchezo huo wa ufunguzi utafuatiwa na Mali dhidi ya Burkina Fasso, mechi zote zikichezwa leo.

Taifa Stars, wawakilishi wa Tanzania watashuka uwanjani Januari 19 dhidi ya Zambia, mchezo unaotazamiwa kuwa wa kisasi.

Mchezo wa ufunguzi dhidi ya Zambia unaweza kuwa fursa nzuri kwa Taifa Stars kulipa kisasi kwa Zambia iliyowanyima tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali kwenye fainali za 2009 walipokutana katika mchezo wa mwisho wa Kundi A.

Stars ikihitaji ushindi wa aina yoyote ile katika mchezo huo ili iwe na pointi sita ambazo zingeipeleka nusu fainali, ililazimishwa sare ya bao 1-1 ambayo iliifanya imalize ikiwa nafasi ya tatu na kuishia katika hatua hiyo ya makundi.

Stars iliyopangwa katika Kundi D, ambalo mechi zake zitachezwa jijini Limbe huko Cameroon, kibarua chake cha kwanza kitakuwa dhidi ya Zambia, Jumanne ijayo na kisha Januari 23 itavaana na Namibia na mchezo wake wa mwisho utakaochezwa Januari 27.

Kocha wa Stars, Etienne Ndayiragije alisema kuwa mashindano hayo ni nafasi muhimu na nzuri kwa wachezaji wake kuonekana na kujitengenezea fursa ya kuonwa na timu mbalimbali nje na ndani ya bara la Afrika.