Kisa Yanga, Ihefu yaoga noti, yaahidiwa ndege

USHINDI raha sana buana asikwambie mtu, kwani unaambiwa baada ya kuizima Yanga juzi mastaa wa Ihefu wametembezewa mkwanja ikiwa ni motisha ya kuwapa nguvu na morari kuhakikisha mechi zinazofuata wanaendeleza moto na kujinasua nafasi za chini.
Ihefu imekuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga ambayo ilikuwa imeshindikana ikicheza mechi 49 za ligi kuu bila kupoteza na kujikuta ikiacha pointi tatu kwenye uwanja wa Highland Estate uliopo wilayani Mbarali mkoani hapa ilipofungwa mabao 2-1.
Ushindi huo ulikuwa wa tatu kwa Ihefu msimu huu na kuwafanya kujinasua mkiani hadi nafasi ya 13 kwa pointi 11 na sasa inajiandaa na mchezo ujao dhidi ya Kagera Sugar huko jijini Mwanza kumaliza mzunguko wa kwanza.
Habari ilizopata Mwanaspoti kutoka kwa mastaa wa Ihefu, zilisema baada ya ushindi huo mabosi walionesha tabasamu na kuwamwagia pesa ikiwa ni kuwapongeza kwa kazi nzuri.
Ilielezwa kuwa kabla ya mechi, mkurugenzi wa timu hiyo, Fahadi Haroon alikuwa ameahidi Sh 30 milioni kwa wachezaji kama watashinda, ambapo baada ya mchezo alikuja na mabadiliko akiongeza mkwanja mwingine.
“Baada ya mechi akasema mnaonaje niongeze nyingine, tukaamsha shangwe akaongeza kibunda kama Sh 10 milioni nyingine, akasema hata safari ya Mwanza kucheza na Kagera Sugar tutaenda na ndege, japo ndege ndio imezingua,” alisema mmoja wa wachezaji kikosini humo.
Akizungumza hilo, katibu mkuu wa timu hiyo, Zagalo Chalamila alikiri vijana kupewa mshiko, akifafanua kuwa huo ni utaratibu wao wa kila mechi na kwamba hata baada ya mchezo dhidi ya Yanga, pesa iligawiwa kwa nyota wao.
Alisema ushindi huo uliwapa raha sana hata viongozi kwani Yanga ilikuwa haijapoteza muda mechi yoyote ligi kuu kwa muda mrefu, hivyo nyota wao lazima wapongezwe.
“Sisi ndio utaratibu wetu kila mechi japokuwa tulifurahi kuwa timu ya kwanza kuwasimamisha Yanga waliokuwa ‘unbeaten’ mechi 49, vijana walifanya vizuri tukawapa kifuta jasho,” alisema Chalamila bila kutaja kiwango