Kisa Saido… Kaze awaka Yanga

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kuanza safari ya kwenda jijini Tanga kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, lakini Kocha Mkuu wake, Cedric Kaze amewaka kisa ni nyota wake wawili Saido Ntibazonkiza na kitasa Dickson Job waliokuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Saido na Job walisajiliwa kwenye dirisha dogo, japo mshambuliaji huyo kutoka Burundi alishaanza kuitumikia timu hiyo tofauti na mwenzake, wote walikuwa majeruhi na kushindwa kuitumikia timu yao, lakini juzi kati wameitwa kwenye timu za taifa za Burundi na Tanzania kwa mechi za kimataifa.

Kitendo hicho kimemchefua Kaze, akidai kujumuishwa kwa wachezaji hao katika timu hizo za taifa wakiwa bado hawajawa fiti, kimemchanganya.

Job ameitwa kikosi cha Tanzania, Taifa Stars na Kocha Kim Poulsen kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Kenya na nyingine mbili za kuwania kufuzu fainali za Afrika (Afcon) 2022, huku akiwa hajaichezea klabu yake mechi yoyote tangu asajiliwe kwa sababu ya majeraha.

Job aliumia kwenye kambi ya Stars, ikijiandaa na michuano ya Chan 2021, iliyomalizika hivi karibuni nchini Cameroon, wakati Saido ameitwa kwenye timu ya taifa lake la Burundi.

Kaze alisema baada ya Job kuumia alitibiwa na Yanga, hivyo kocha Poulsen alipaswa kuwasiliana naye ili kupata taarifa ya mchezaji huyo.

“Job ndio kwanza ameanza mazoezi ili kujiweka fiti tayari ameitwa tena, wakati hajacheza mechi hata moja, simpingi kocha Poulsen pengine anataka kumuangalia kwa karibu, lakini hilo halizuii kupata taarifa kutoka kwangu ili kumpa programu zake ili akirejea ndani ya timu asianze upya,” alisema Kaze aliyedai pia anashangaa Saido naye akiwa hajacheza karibu miezi miwili, ghafla naye anaitwa timu ya taifa.

“Saido ni majeruhi hajacheza muda mrefu najiuliza mbona kaitwa kwenye timu yake ya taifa, laiti kama makocha wangeniuliza ningewapa taarifa za wachezaji hao,” alisema Kaze akihofia anaweza akaumia tena na kushindwa kumtumia wakati timu yake inahaha kusaka mabao.

Kaze alikiri kwamba timu yake ina changamoto ya kufunga mabao kutokana na kukosa mshambuliaji halisi wa kucheka na nyavu.

“Ni kweli wachezaji walioongezwa dirisha dogo sio wabaya, lakini sio wale mastraika halisi kabisa. Pamoja na hilo tusingetumia dirisha hilo kubomoa kikosi na kusajili wachezaji wengi, linatumika kwa ajili ya kuimarisha kikosi, Saido alikuwa tofauti kidogo, naye tunamkosa,” alisema na aliongeza;

“Baada ya kutoka Kombe la Mapinduzi wachezaji wengi ni majeruhi, lakini mechi za mbele watarejea kwenye kiwango chao kupigania malengo ya timu.”

Kuhusu kadi nyekundu aliyoonyeshwa nyota wake, Carlos Stenio ‘Carlinhos’ walipocheza dhidi ya Ken Gold ya Chunya kocha huyo alisema;

“Kwanza mchezaji ndio kwanza alianza kurudi mchezoni baada ya kutoka kuumwa, nitamjenga na kumrekebisha alipokosea. Kuhusu waamuzi sipendelei kuwazungumzia lakini kwa upande wao wakaliangalie hilo, kama wapo sawa ama la.”

Hata hivyo, licha ya Kaze kuwalilia wachezaji wake hao, bado kanuni za Fifa kwa wachezaji wanaoitwa timu za taifa zinambana kwani zinaruhusu wachezaji kuzitumikia timu zao za taifa pale wanapoitwa na ikitokea wamezuiwa, klabu husika na mchezaji huadhibiwa.

Kuhusu mchezo wao wa Alhamisi dhidi ya Coastal Union, Kaze alisema anajua mchezo utakuwa mgumu, lakini anahitaji ushindi tena wa mabao mengi ili kuzidi kulinda rekodi yao ya kutopoteza na kujiimarisha kileleni.

Yanga imekuwa ikipata wakati mgumu ikicheza Mkwakwani Tanga. Hata mechi yao ya mwisho ya msimu uliopita iliisha kwa suluhu, licha ya kupata ushindi inapocheza jijini Dar es Salaam dhidi ya Wagosi wa Kaya.

Mara baada ya mechi hiyo ya Alhamisi, Yanga itasafiri hadi Moshi kucheza na Polisi Tanzania moja ya timu inayowasumbua kila wanapokutana, huku vijana wa Kaze wakitakiwa kukomaa ili kulinda rekodi yao ya kutopoteza katika Ligi kwani tangu walipolazwa 1-0 na KMC Machi 12, 2020 imecheza jumla ya mechi 33 bila kupoteza (mechi 12 za mwisho za msimu uliopita na 21 za msimu huu).