Kipigo cha Yanga champonza Cioaba

Thursday November 26 2020
kocha pic

MABOSI wa Azam FC waliokuwa wamejifungia kufanya kikao kizito jioni hii ya Alhamisi, imetangaza kuachana na kocha mkuu wake, Aristica Cioaba na kocha wa viungo Costantine kwa makubaliano maalum.
Afisa Habari wa Azam, Thabit Zakaria 'Zaka', amethibitisha jioni klabu hiyo kuachana na makocha hao na kwa mechi mbili zijazo dhidi ya Biashara united na Gwambina, timu itakuwa chini ya kocha msaidizi wao, Vivier Bahati, wakati mipango mingine ikipangwa.
Maamuzi ya Azam kuachana na Cioaba kumekuja saa chache tangu timu hiyo kupokea kipigo cha pili mfululizo katika Ligi Kuu Bara.
Azam ilinyooshwa na Yanga bao 1-0 jana usiku kwenye uwanja wa nyumbani ikiwa ni siku chache tangu wafumuliwe na KMC kwa idadi kama hiyo, ikiwa ni kipigo cha tatu kwa timu hizo msimu huu na kukiacha kiti cha uongozi kwa mabingwa hao wa kihistoria.
Zaka alikiri licha ya kwamba wameachana na makocha hao kwa sheria za mikataba, lakini ukweli ni kwamba maamuzi yamefikiwa kutokana na timu kuyumba siku za karibuni tofauti na ilivyooanza msimu kwa kushinda mechi saba mfululizo na kuiongoza msimamo kwa muda mrefu.
Katika mechi nne zilizopita Azam imeambulia pointi nne tu, kwa kushinda mechi moja na sare moja, huku ikipoteza michezo miwili.
Aidha wakati Cioaba akitimuliwa sambamba na Costantine, klabu hiyo imedaiwa imemnyakua mtaalam wa michezo (Sports Scientist) kutoka Zimbabwe, Nyasha Charandura aliyekuwa klabu ya Warriors.
Taarifa za uteuzi huo wa mtaalam huyo zilifichuliwa na Shirikisho la Soka Zimbabwe (ZIFA) ambalo kupitia kurasa wake rasmi wa Twitter, uliweka taarifa ikimpongeza na kumtakia kila la heri kwa kuteuliwa kwake na klabu ya Azam.
"Tunawatakia kila la kheri Azam, wakijua kuwa maarifa yake ya baadaye yataongeza sana ushindani wa klabu yake, Charandura amekuwa na Warriors tangu 2018," ZIFA iliandika.
Hata hivyo Zaka alipoulizwa juu ya Charandura alisema hana hakika nalo, japo anafahamu wapo kwenye mazungumzo na mtu kutoka Zimbabwe, lakini sio kocha wa viungo na taarifa rasmi itatangazwa rasmi baadaye watakapomalizana naye.
Pia alisema kikosi chao kitaondoka jijini Dar es Salaam kesho Ijumaa kwenda Kanda ya Ziwa kwa ajili ya mechi zao mbili, msafara utakakaokuwa na watu 35 wakiwamo wachezaji 22 chini ya Kocha Bahati ambaye ni raia wa Burundi.


Advertisement