Kina Banda kazi kazi tu

KUNA wanandugu wanaocheza soka ndani na nje, wamezungumzia wanapokutana wanashauriana namna ya kufanya kazi kwa ubora utakaowapa michongo ya maana, itakayofanya wafurahie vipaji vyao.

Abdi Banda beki wa Chippa United ya Afrika Kusini ana mdogo wake ambaye ni kiungo wa Coastal Union ya Tanga, Omary Banda alisema wanapozungumzia kazi wanaweka utani pembeni na kuangalia namna wanavyoweza kufanya makubwa kwenye soka.

“Kama sijabanwa na majukumu ya timu yangu, napenda kumwangalia mdogo wangu anapocheza mechi ili nijue ubora na udhaifu wake, lakini jambo la msingi zaidi namsisitiza nidhamu ya mazoezi itakayomfanya muda wote awe fiti.

“Soka halina kificho mchezaji anayekuwa amejiandaa kazi yake inakuwa inajidhihirisha, pia najitahidi niwe mfano kwake ili kumuwekea misingi ya kufika mbali zaidi bila kutembelea jina langu,”alisema.

Wakati winga wa Al-Qadsiah ya Saudi Arabia,Mtanzania Simon Msuva alisema mdogo wake James Msuva anayekipiga Mbeya City anamshauri kukiamini kipaji chake na kuongeza bidii katika majukumu yake, kitu kitakachomfanya afurahie matunda ya soka.

“Tukikutana kuna wakati tunaweka marudio ya kazi zetu, kisha tunashauliana namna ya kuzifanya kwa kiwango kitakachotupa thamani kubwa,” alisema.