Kilichowakuta Morrison na Ajibu

Thursday April 08 2021
morrison pc
By Olipa Assa

UBORA wa Simba, umeonekana ni kikwazo kwa mastaa wa timu hiyo, Benard Morrison, Ibrahim Ajibu na Gadiel Michael, kufurukuta mbele ya washindani wao, hivyo wamepewa namna ya kujinasua.

Mchezaji wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala alimtolea mfano Morrison kwamba katika namba yake yupo Luis Miquissone ambaye ni mbunifu wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao hadi sasa ana pasi tisa alizowatengenezea wengine waliofunga, kwamba bila staa huyo raia wa Ghana kujituma anaweza akajikuta anaishia kufanya kazi ndogo, japokuwa kwa ubora.

“Bado Morrison ni mchezaji mzuri sana ndio maana hata muda mdogo anaopewa anafanya vitu bora, lakini anapaswa kuonyesha vitu vyake mbele ya Luis na Chama ambao wana njaa ya kufunga mabao na watafutaji,” alisema.

Alisema Simba ya sasa inaifunga timu yoyote ndani ya dakika 90 na kuzishauri zile ambazo zitakutana nayo kwenye ligi kwamba wanatakiwa kucheza kwa tahadhari na sio kuibeza.

“Simba inatia hofu ikicheza na mpinzani, kwanza katika ligi kuu ina safu nzuri ya ushambuliaji ambayo ndani ya dakika 90 mpinzani ni ngumu kusalimika, ukweli ndio utazifanya timu nyingine zijipange vyema kutengeneza timu za ushindani ili soka liwe na burud ani,”alisema.

Kauli yake iliungwa mkono na mchezaji wa zamani wa Simba, William Martin kwamba ubora wa kikosi cha timu hiyo, mchezaji anayepata nafasi anafanya na majukumu ya mwingine, hivyo ushauri wake kwa Ajibu, Gadiel na Morrison ni kwamba wanapaswa kupambana mazoezini zaidi ya wale wanaopangwa kikosi cha kwanza na kocha Didier Gomes.

Advertisement

“Katika mazoezi wanatakiwa wawe wabunifu kwasababu timu inanolewa na mzungu anayeangalia anayefaa kwa wakati huo, ni wachezaji wazuri wasikubali kushusha mikono chini kuona wameshindwa kupambana kikosi cha kwanza bado wana nafasi na ni wachezaji wakubwa,”alisema.

Naye beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima alisema kuna haja kwa wachezaji hao kujitathimini wenyewe kujua Simba ni ya aina gani kwasasa, ili waweze kukuza thamani ya viwango vyao na sio kuridhika.

“Mfano wachezaji wazawa kama Ajibu na Gadiel ni wachezaji ambao awali walikuwa nguzo muhimu kwenye timu ya Taifa Stars, lazima wajipambanue vya kutosha kujua soka ni la ushindani wa hali ya juu wasitembee na historia ya nyuma,” alisema.

Advertisement