Kigonya: Huyo Aucho si mchezo

Sunday September 26 2021
aucho pic
By Waandishi Wetu

KIPA namba moja wa Azam FC, Mganda Mathias Kigonya amewapa kongole viongozi wa Yanga kunasa saini ya kiungo mkabaji, Khalid Aucho na kuweka wazi kuwa wapinzani wana kazi nzito kumkaba.

Kigonya aliliambia Mwanaspoti kuwa ameshuhudia usajili mkubwa timu zote msimu huu na anatarajia ushindani mkubwa kutokana na ubora wa mchezaji mmoja mmoja na maandalizi ya timu, lakini Aucho kutua Yanga imemshangaza na kuwaona viongozi wa timu hiyo wapo makini kwenye uchaguzi wa wachezaji.

“Kila timu imefanya usajili kulingana na mahitaji na malengo ya timu zote mwanzoni mwa msimu ni kutwaa taji. Wapinzani wamefanya usajili, Azam pia wamefanya usajili mzuri tena wa ushindani lakini ninachoweza kuzungumza kwa wapinzani ni usajili wa Aucho kutokana na kumfahamu,” alisema Kigonya.

“Ni mchezaji mzuri nimewahi kucheza naye kwenye timu ya taifa Uganda. Namfahamu ni moja ya wachezaji bora niliowahi kuwashuhudia hususan viungo na ataisaidia timu kama watamtumia vizuri.”

Akizungumzia mipango yake kuelekea msimu mpya, alisema atahitaji kushindanishwa na makipa wengine kwa sababu anaanza nao pamoja na malengo yake ni kuibuka kipa bora wa msimu.

“Nilifika katikati ya msimu sikuona sababu za wengi kunilinganisha na makipa niliowakuta. Sasa nawaambia Mimi ndiye kipa bora kwenye ligi inayoanza Septemba 27. Nimejipanga kufanya kilicho bora kutokana na ubora nilionao,” alisema.

Advertisement

“Sijisifii na sipendi kuwa muongeaji, nafurahia kucheza nafasi ya kipa kwa sababu nilishapata nafasi ya kucheza ndani (mshambuliaji) na niwapo golini najua mchezaji huyu anataka kufanya nini kwa wakati gani, nadhani hicho ndio kinanipa ubora.”

Kipa huyo aliyetua Azam akitokea Forest Rangers ya Zambia msimu uliopita, alisema anawaheshimu makipa kwani kila mmoja ana ubora na kukazia kuwa yeye ni mchezaji tofauti kuliko wote kwani amewasoma na anatambua ubora na udhaifu wao, hivyo anajiona ni wa tofauti.

IMEANDIKWA NA RAMADHAN ELIAS, CHARITY JAMES NA DAUDI ELIBAHATI

Advertisement