Kiduku: Pambano la Misri! lilikuwa ni mazoezi tu

TWAHA 'Kiduku' Kassim amerejea nchini alfajiri ya leo Jumapili akitokea Misri alikochapwa kwa pointi na Ulugbek Sobirov wa Uzbekistan, pambano ambalo anadai lilikuwa kama mazoezi tu kwake.

"Ni kama nimecheza sparing' mazoezi ya kuzichapa ana kwa ana' mpinzani wangu hakuwa bondia wa kitoto, ila nimejikaza hadi kumaliza raundi zote 10," Kiduku ameiambia MCL Digital, muda mfupi baada ya kurejea nchini.

Katika pambano hilo lililopigwa kwenye ukumbi wa Fitbox Gym, Club 7, Katameya Hills, New Cairo, Kiduku alipigwa kwa pointi huku zikiibuka taarifa kwamba bondia huyo ameumizwa bega na kuwahishwa hospitali nchini humo.

"Niko salama na nimerejea nyumbani salama, leo saa 4 asubuhi nilianza safari ya kuelekea Morogoro nikiwa salama kabisa, " amesema bondia huyo ambaye aliwasili kwenye uwanja wa Nndege wa Dar es Salaam (JNIA) alfajiri ya leo.

Wasiwasi kwa mashabiki wa ndondi ni je? Kiduku atasalia na nyota zake mbili na nusu au ataporomoka kwenye ubora wa ndondi ndani na nje ya nchi baada ya kipigo hicho?.

"Hiyo inategemea na namna Boxrec 'mtandao wa viwango vya dunia wa ngumi za kulipwa' katika kuingiza pointi, kama amepigwa na bondia ambaye alikuwa chini yake kwenye renki kiuhalisia lazima anyang'anywe pointi," anasema Anthony Rutha bondia wa zamani na refarii wa ndondi nchini.

Kabla ya pambano hilo, Kiduku alikuwa na nyota mbili na nusu na mpinzani wake alikuwa na nyota mbili.

"Hiyo nusu nyota ya Kiduku lazima iondoke, mpinzani wake atapanda kwenye ubora," anasema.

Hata hivyo, habari zaidi zinasema Kiduku ameingiza si chini ya Sh 40 Milioni, ingawa mwenyewe hajataka kuweka wazi pesa aliyolipwa kwenye pambano hilo.