Kiduku, Mcongo warushiana maneno 

Wednesday April 07 2021
ngumi pc
By Imani Makongoro

Saa chache kabla ya kumaliza ubishi wa nani mkali ulingoni, mabondia Twaha 'Kiduku' Kassim na Tshibangu Kayembe wa DR Congo wameingia katika vita ya maneno kila mmoja akijinasibu kushinda Ijumaa ya April 9 katika pambano lao litakalofanyika kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza Dar es Salaam.
Kiduku amemwambia  Kayembe wa DR Congo kuwa asitarajie ushindi kwenye pambano hilo la raundi 10 la uzani wa kati.
Kayembe  ambaye aliwahi kuchapwa na mtanzania Hassan Mwakinyo kwa pointi za majaji wote mwaka jana ni bondia namba tatu nchini mwake  pia akishika nafasi ya 284 kati ya 1650 duniani kwenye uzani wake. 
Mabondia hao kesho Alhamisi watapima uzito na afya tayari kupanda ulingoni Ijumaa, pambano lililoteka hisia za mashabiki  za mashabiki wengi.
"Alicheza vipi au alipigwa vipi na Mwakinyo hiyo sitaki kujua, lakini niwambie tu mashabiki wangu kwamba nitacheza 'boxing' ya burudani," amesisitiza Kiduku.
"Kwa matokeo ya aina yoyote ile Kayembe nitampiga, iwe kwa pointi au KO lakini lazima ajiandae kwa kipigo atake asitake," amesema Kiduku.
Kayembe amejibu mapigo akisisitiza kwamba amekuja nchini kwa kazi moja tu, kumchapa Kiduku na kuweka rekodi ya kushinda hapa nchini.
"Mara ya mwisho kucheza Tanzania nilipoteza kwa pointi, nilijua sababu ni kumlea lea mpinzani wangu hadi tukamaliza raundi zote, sasa kwa huyu Kiduku, ajipange haswa,"  amesema Kayembe.

Advertisement