Kichuya anasemaje...?

NYOTA wa zamani wa soka nchini wameelezea sababu za kushuka kwa kiwango cha winga wa Namungo FC, Shiza Kichuya huku yeye akisema bora hata anavyopata dakika chache za kucheza kuliko angekuwa anatupwa jukwaani.

Ndani ya kikosi hicho, Kichuya hajawa chaguo la kwanza tangu timu hiyo ikiwa chini ya hiyo Thiery Hitimana na sasa Hemed Suleiman ‘Morocco’.

Aliyekuwa beki wa Yanga, Bakari Malima alisema “Hata kama alikuwa hapati nafasi ya kucheza, alitakiwa kuangalia timu nyingine nje ya nchi na sio kurudi Tanzania, kitendo cha kurudi hapa anaonekana kama anacheza kijanja hana kiwango kama kile alichokuwa nacho wakati yupo Simba, anacheza kawaida tu kwa sasa.”

Naye mshambuliaji wa zamani Yanga, Herry Morris alisema, “Kiwango kweli kimeshuka lakini sio sana, nimemwona akicheza mechi chache na akiingia anaonyesha kitu cha tofauti, nadhani hana bahati Namungo.”

Kwa upande wa straika wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema; “Kwa sasa ameporomoka labda kutokana na kukaa benchi, lakini umri wake una ruhusu kufanya marekebisho na kurejea kiwango chake, kushuka kwa mchezaji ni vitu vya kawaida kikubwa ni kujitambua.”

Wakati nyota hao wanaelezea kiwango chake, Kichuya alisema anaona bora kwa dakika 10 au 15 anazocheza kuliko kukaa benchi kabisa ama kukosa nafasi ya kucheza.

“Kwangu licha ya watu kuniambia bado nafanya vizuri na wengine sifanyi vizuri, huwa naangalia zaidi kile ninachoambiwa na kocha wangu na kukifuata uwanjani, pia najitambua na najua nini ambacho nakifanya.”