Kibarua cha kwanza kwa Mfaransa

MICHUANO ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 16 bora inaendelea kurindima tena kesho kwa mchezo mmoja kupigwa ambapo Singida Fountain Gate itakuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuikaribisha Tabora United.

Tabora inaingia katika mchezo huo ikiwa chini ya kocha mpya Mfaransa, Denis Laurent Goavec ikiwa ni mechi yake ya kwanza tangu atambulishwe ndani ya kikosi hicho Machi 22, mwaka huu akichukua nafasi ya Mserbia, Goran Kopunovic aliyetimuliwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Goavec alisema licha ya ugeni wake nchini haitakuwa ngumu kwake kutokana na maandalizi yao.

"Tumekuwa na kipindi bora cha kufanya mazoezi na wachezaji wote wako kwenye morali kubwa isipokuwa tutamkosa mchezaji wetu, Cletus Emotan anayesumbuliwa na majeraha ya nyonga hivyo ataungana na wenzake siku chache zijazo," alisema.

Kwa upande wake, kocha mkuu wa Singida, Jamhuri Kihwelo 'Julio' alisema, licha ya kukaa kwa muda mrefu bila ya kucheza wao kama benchi la ufundi na wachezaji wamejipanga vizuri huku akiweka wazi anatarajia kukutana na ushindani mkubwa.

Singida ilitinga hatua hiyo baada ya kuifunga FGA Talents mabao 2-0 huku Tabora ikiitoa Nyamongo ya Mara kwa kuichapa pia 2-0.

Hadi sasa timu pekee iliyotinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ni Namungo iliyoitoa Kagera Sugar kwa mikwaju ya penalti 5-3, baada ya kutoka suluhu ndani ya dakika 90, katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa Ruangwa Lindi.