KIBANDA UMIZA: 'Simba wakirudi nitalala wapite juu'

FURAHA ikizidi inaweza kukufanya uropoke tu. Wazee wa kibanda umiza tulipata nafasi ya kusafiri hadi maeneo ya Kivule kushuhudia mchezo kati ya Simba na US Gendarmerie uliopigwa wikiendi iliyopita nchini Niger.

Na baada ya dakika 90 kumalizika kwa Simba kupata alama moja muhimu ugenini, jamaa mmoja wa makamo aliamua kutia fora kwa jinsi mzuka ulivyokuwa umempanda.

Akiwa anatoka kibandani alionekana akishangalia kwa kurusha rusha mikono kwa nguvu huku akisonya kwa furaha.

“Aaah kwa Simba hii, mende gani atakuja mbele yetu tumuache, sijui tujitoe kwenye ligi?” (Akimaanisha Ligi Kuu Bara) ..“nawaambiaje.. hawa wakirudi nataka niende uwanja wa ndege pale nilale wachezaji wa Simba watembee juu yangu..”

Kauli yake ya mwisho ilizua shangwe kwa baadhi ya mashabiki wa Simba lakini miongoni mwao pia kulikuwa na shabiki wa Yanga ambaye alisikika akiongea kwa sauti ya chini huku akiondoka: “Sasa si utaahira huo...”