Kenya yafuzu fainali za Kombe la Dunia

NAIROBI. TIMU ya taifa ya wanawake ya voliboli ya ufukweni imetunukiwa tiketi ya moja kwa moja kushiriki fainali za Kombe la Dunia (FIVB) mwaka huu.

Vipusa hao wa kocha, Salome Wanjala wamepata nafasi hiyo wiki mbili baada ya kutunikiwa tiketi ya kushiriki kipute cha Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa kuibuka kati ya nafasi tano bora kwenye msimamo wa fani hiyo duniani kwa mataifa yaliyo chini ya mwavuli wa michezo ya Madola.

Shirikisho la Voliboli Duniani (FIVB) limesema hakuna mechi za kufuzu zitakaondaliwa maana muda ni mchache. Fainali za Kombe la Dunia zitafanyika Juni 10 hadi 19 mwaka huu jijini Roma, Italia. Nayo Michezo ya Jumuiya ya Madola itafanyika Julai 29 hadi Agosti 8 chuo kikuu cha Birmingham, Uingereza.

Kwenye fainali za Kombe la Dunia, Kenya itakuwa kati ya mataifa manne yatakayowakilisha Afrika. Mataifa mengine ni Misri, Morocco na Msumbiji.

“Bila shaka tunashukuru zaidi kwa maendeleo hayo hii ikiwa ni baada ya kuibuka nafasi ya tatu kwenye mechi za kuwania tiketi ya Jumuiya ya Madola zilizoandaliwa nchini Ghana mwezi uliyopita,’’ kocha Wanjala alisema.