Ken Gold yatambulisha uzi mpya

Muktasari:

Timu hiyo inajiandaa na michuano ya Championship (zamani Daraja la Kwanza) ambapo itaanzia ugenini Oktoba 2, mwaka huu dhidi ya Pamba katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

TIMU ya Ken Gold ya Chunya mkoani Mbeya leo imetambulisha rasmi jezi zake itakazotumia kwenye michuano ya Championship na Kombe la Shirikisho (FA) msimu huu.

Utambulisho huo umefanyika jijini Mwanza ambapo jezi ya nyumbani itakuwa na rangi ya njano, ya ugenini rangi ya bluu na jezi ya tatu itakuwa na rangi ya kijani.

Ken Gold imetambulisha jezi hizo baada ya kuingia makubaliano ya udhamini wa vifaa vya michezo na kampuni ya SML Laboratory ya hapa nchini.

Akizindua jezi hizo Boniphace Heche amesema ni jambo jema kuona timu za chini zinapewa nguvu na kuaminika huku akitoa rai kwa wadau wengine kusapoti na kusaidia kunyanyua vipaji kwenye ligi za madaraja ya chini.

Mkurugenzi Mtendaji wa SML Laboratory, Simon Shinji amesema udhamini huo ni wa mwaka mmoja ambao utahusu vifaa vya michezo na utawala kwa kusaidia fedha za uendeshaji ili kuhakikisha timu inashiriki Ligi katoka mazingira rafiki.


"Mkataba wetu ni wa mwaka mmoja una vipengele viwili kwenye vifaa vya michezo na utawala, tunaaka kuona timu inasafiri bila wasiwasi kwenda kwenye mechi zake na ina vifaa vyote vinavyotakiwa, tunahamasisha wadau wengine wasibague wakajikita tu Ligi Kuu washuke huku chini timu hizi zinahitaji kuungwa mkono," amesema.

Katibu wa Ken Gold, Ethan Benson amesema uwepo wa udhamini huo ni jambo zuri kwani unaisaidia klabu kufanya shughuli zake kwa utulivu na kujiamini ili kufanikisha mipango yake ya kupanda daraja kwenda Ligi Kuu.