Kaze: Unbeaten ina heshima

KOCHA msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema kutofungwa kwao mechi 48 ni heshima kubwa kwao na mashabiki wa timu hiyo kwa misimu miwili mfululizo.

Yanga ni timu pekee ambayo haijapoteza mechi hizo hali ambayo inawafanya mashabiki na hata wachezaji wao watembee kifua mbele kwasasa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari,  Kaze amesema siri ya kutopoteza kwao inatokana na kuchukulia umuhimu wa kila mchezo wao kwenye Ligi.

"Siri yetu ni kufanya mazoezi yale yale kwenye kila mchezo bila kuangalia tunakutana na  nani, lengo letu ni kuchukua pointi tatu ili kwenda mbele zaidi katika Ligi," amesema Kaze.

Akizungumzia mchezo huo, kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema  wanajua wanaenda kukutana na Mbeya City ambao ni mshindani mgumu lakini wamejianda vizuri kuhakikisha wanapata pointi kwenye mchezo huo.

Kaze amesema Mbeya City ina matokeo mazuri ambayo yanawabeba wakiingia kwenye mchezo huo ambao utakuwa mgumu kutokana na rekodi ya timu hizo mbili zinapokutana.

"Msimu uliopita tulitoka nao sare kwenye uwanja wa Mkapa ni timu nzuri, kesho kutakuwa na mabadiliko kwenye kikosi chetu kwa sababu tumecheza mechi nyingi  kwahiyo wachezaji wengine watahitaji kupumzika,"alisema Kaze na kuongeza;

"Wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za Taifa wamerejea na wale ambo walikuwa kwenye adhabu pia wamerejeo kwahiyo ni kitu kizuri kwetu."

Kaze amesema anatambua Mbeya City ni timu ambayo inakuwa inacheza kwa spidi muda wote wa mchezo na hilo ni kutokana na ufiti ambao wachezaji wanao.

"Mbeya City ni tofauti na timu nyingi kwa sababu dakika 90 zote huwa wapo vile vile hawapoi, sisi tumejiandaa vizuri na tunaamini tutafanya vizuri kwa kile tulichokiandaa," alisema Kaze.