Kaze arejea rasmi Yanga

Muktasari:

YANGA wamefanya uamuzi mgumu. Wameamua kumrejesha kwenye benchi la ufundi la klabu hiyo Kocha Mrundi, Cedrick Kaze.

YANGA wamefanya uamuzi mgumu. Wameamua kumrejesha kwenye benchi la ufundi la klabu hiyo Kocha Mrundi, Cedrick Kaze.

Habari za awali ambazo Mwanaspoti imejiridhisha nazo ni kwamba anakuja kuwa msaidizi wa Nasreddine Nabi ambaye awali alikuwa na mtihani wa kushinda mechi dhidi ya Rivers ugenini na ile ya Simba Jumamosi kulinda kibarua chake.

Mbali na Kaze pia inatajwa Yanga wako kwenye mazungumzo na Mwinyi Zahera ambaye yeye anaweza kupewa pia nafasi hiyo au Ukurugenzi wa Ufundi aisuke Yanga idara zote.

Habari za ndani zinasema kuna kundi linamtaka Zahera kutokana uwepo wa Wakongomani wengi ndani ya kikosi hicho ambao amefanya nao kazi kwa nyakati tofauti kwa mafanikio ingawa wapo wanaomtaka zaidi Kaze kwa madai kwamba anacheza soka la kisasa.

Mtihani wa kwanza wa Kaze Yanga utakuwa ni dhidi ya Simba utakaopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo Yanga wanataka matokeo zaidi ya kitu chochote duniani kwa sasa.

“Tuna imani na Kaze na tunaamini ataongeza nguvu kwa Nabi kujua ni mbinu gani zinaweza kuwafanya wakawa bora ndani baada ya kushindwa kufanya vizuri kimataifa,” alidokeza kiongozi mmoja.

“Tumepoteza nafasi mapema sana hatukuwa na lengo hilo mipango ilikuwa ni kufanya vizuri na kufika hatua kubwa lakini imeshindikana baada ya kutolewa hatua ya awali sasa tunahamia Ligi Kuu.”

Akizungumzia kambi ya timu alisema leo wanaingia kambini kwaajili ya kuendelea na maandalizi na wachezaji wameshapewa taarifa kuwa watakuwa na ugeni wa kocha mpya wanahitaji kumpa ushirikiano ili waweze kufikia malengo.

Kaze uraia wa Burundi alishawahi kuinoa Yanga msimu uliopita akirithi mikoba Krmpotick hakufanya kazi muda mrefu akaondolewa kikosini humo kutokana na kushindwa kufikia malengo.

Kaze, 40, amekuwa akitajwa kama miongoni mwa kocha bora katika umri wake ambapo katika umri huo tayari ameshazinoa timu kama Prince Louis Rwagasore Fc, timu za taifa la Burundi katika umri wa U17, U20 na U23.