Kaze ajiweka mtegoni kushinda mechi saba TU!

Friday November 20 2020
kaze pic

KOCHA bora wa mwezi Oktoba, Cedric Kaze, amesisitiza kwamba ndani ya mechi saba zijazo atakuwa na mwanga juu ya uamuzi sahihi anaopaswa kufanya Yanga kwenye dirisha dogo.

Kaze, ambaye anajiandaa kuikabili Namungo Jumapili Jijini Dar es Salaam, alisema kuazia mechi hiyo anajipa michezo saba tu ambayo ni sawa na dakika 630.

Kocha huyo raia wa Burundi aliyewahi kunoa timu za taifa lake za soka karibu zote, ameliambia Mwanaspoti atatumia michezo hiyo kuwapima mastaa wake kama wapo ambao, wataweza kumshangaza na kubadilika katika viwango bora kama anavyotaka au anahitaji kuwaweka pembeni.

“Kuna kitu ambacho nafikiria kufanya katika timu,” alisema Kaze ambaye leseni yake ni kubwa kuliko za makocha wote wa kigeni waliopo kwenye Ligi za Bongo.

“Ukiangalia tuna kama mechi saba hapa za kucheza kumaliza mzunguko wa kwanza ni mechi nyingi ambazo pia zinaweza kubadilisha vitu vingi kwasasa tunataka kuelekeza akili yetu katika mechi hizo,” aliongeza kocha huyo ambaye anapenda soka la kushambulia.

kaze1 pic
Advertisement

Alisema anatambua mzunguko wa pili utakuwa mgumu lakini kabla ya hapo atakuwa ameshakutana na mabosi wake kuangalia wapi wajiimarishe katika mbio za ubingwa ambao amekiri kuupania.

“Tukianza kuelekea ukingoni wa mechi hizo saba tutakutana na viongozi tuwakabidhi ripoti yetu ya wapi tunahitaji kuiboresha timu yetu ili iwe katika ubora zaidi wa kufikia malengo yetu.

“Tuna uhakika kwamba mzunguko wa pili utakuwa mgumu sana kwa kila timu kila timu itataka kujiimarisha zaidi ili ziweze kuwa vizuri kufikia malengo ya kucheza mashindano ya Afrika na hapo ndipo ugumu na umuhimu wa kujipanga utakuja,” alisema na kusisitiza kwamba mechi mbili zilizopita walizotoa sare walitakiwa kushinda ila walikosa watu sahihi wa kumaliza mechi.

“Mechi mbili zilizopita bado naamini tulipaswa kupata pointi zaidi ya hizi tulizopata ukiangalia kama mechi ya Simba wakati wanatushambulia tuliamini kwamba tungepata nafasi.

“Lakini tulikosa watu bora ambao wangeweza kupiga pasi za kumaliza mchezo. Kama makocha tumeliona hilo na sasa tunataka kutumia makosa hayo kujiongezea uzoefu wa kujipanga zaidi kwa mambo tunayotaka kuyaboresha ndani ya timu yetu.

“Hatukuwa na mtu ambaye angeweza kutengeneza utofauti kati yetu na wapinzani usipotumia nafasi kama hiyo unampa nafasi mpinzani kufikiria anaweza bado kupambana na wewe,” alisema Kaze ambaye alifanya kazi kwa mafanikio kwenye akademi ya Barcelona inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania.

______________________________________________________________

Na KHATIMU NAHEKA

Advertisement