Kaseke sio wa mchezo mchezo, awapa raha Wananchi

Muktasari:

NYOTA wa Yanga SC, Deus Kaseke ameendelea kuwa moto wa kuotea mbali kwenye mchezo wake wa pili mfululizo Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifungia bao timu hiyo ya Wananchi kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania.

NYOTA wa Yanga SC, Deus Kaseke ameendelea kuwa moto wa kuotea mbali kwenye mchezo wake wa pili mfululizo Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifungia bao timu hiyo ya Wananchi kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania.

Katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam Kaseke alianza kuonyesha makali yake kwa kuifungia Yanga bao pekee lililowafanya Wananchi kuondoka na pointi tatu  kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Akianza kwa mara pili mfululizo kwenye kikosi cha Cedrick Kaze, Kaseke alionyesha kuwa kocha huyo hakufanya makosa kumuanzisha kwa kupachika bao la kuongoza kwa Yanga dakika ya 32 akimalizia pasi ya Yacouba Sogne.

Yacouba aliipenyeza pasi ya chini chini kwa Kaseke ambaye alikuwa akicheza mbele sambamba na Ditram Nchimbi, alichokifanya ni kuchagua tu mpira ule ukwamishe wapi kwenye nyavu za Joseph Ilunda.

Kaseke ameonekana kuwa mzuri zaidi katika umaliziaji tofauti na Nchimbi ambaye amepoteza nafasi kadhaa ambazo pengine zingeifanya Yanga kuongoza katika kipindi cha kwanza kwa idadi kubwa ya mabao.

Asissti aliyotoa Yacouba kwa Kaseke ni ya pili mfululizo, ikumbukwe kuwa nyota huyo wa kigeni ndiye aliyetengeneza bao la Yanga kwenye mchezo uliopita dhidi ya Azam.

Katika kipindi cha pili, Yanga ilianza kwa kushambulia huku Jkt ikijilinda, lakini mambo yaliharibika katika dakika 20 za mwisho ambapo Jkt ndio iliibuka upya na kuanza kulisakama lango la yanga.

Hata hivyo licha ya kushambulia mara kadhaa hakuna walichoambulia kwa sababu hadi dakika 90 zinamalizika ubao ulikuwa ni 1-0.

Matokeo hayo yameifanya Jkt kushuka hadi nafasi tya 16 ikiwa imecheza mechi 13, ikishinda mbili sare na kufungwa saba,ikikusanya jumla ya alama 10. Huku Yanga ikiendelea kusalia kileleni ikifikisha alama 31, ikiwa imecheza mechi 13, ikishinda nane na sare mbili.

Na ELIYA SOLOMON