Kanoute, Onyango freshi

Tuesday September 28 2021
kanoute pic
By Thobias Sebastian

MASHABIKI wa Simba hawana haja ya kuendelea kuwa na presha juu ya nyota wao wawili walioshindwa kumaliza pambano lao dhidi ya Yanga juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam baada ya kuumia, kwani hali zao zipo freshi na kazi zinaendelea kwao kama kawaida.

Nyota hao, kiungo kutoka Mali, Sadio Kanoute na beki kisiki kutoka Kenya, Joash Onyango waliumia kila mmoja kipindi kimoja na kutolewa na Kocha Didier Gomes na kuleta hofu kwa mashabiki, hasa kwa Onyango aliyekuwa akivuja damu usoni, huku chama lao likipasuka kwa Yanga kwa bao 1-0.

Onyango aliumia kipindi cha kwanza na kutolewa nafasi yake ikichukuliwa na Kennedy Juma kisha Kanoute kuumia tena kipindi cha pili na taarifa zilizokuja baadaye uwanjani hapo kwamba wawili hao waliwahishwa hospitalini kwa matibabu zaidi na kuleta hofu kwa mashabiki wa timu hiyo.

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya Simba ni kwamba Onyango aliyesuka eneo la usoni alipata huduma ya kwanza na hali yake sio mbaya sana, sawa na ilivyo kwa Kanoute aliyeumia bega na kwamba wote wanandelea vizuri.

Kanoute alipelekwa hospitali ya Kairuki na kufanyiwa vipimo na kubainika alipata maumivu makali bega la kulia, bahati nzuri hajatenguka.

Majibu yake yalionyesha Kanoute alipata mshtuko wa bega ndio maana alikuwa anasikia maumivu na kushindwa kuendelea na mechi, baada ya kubainika alipatiwa matibu na kuruhusiwa kurudi kambini, japo alikuwa katika hatihati ya kuondoka na kikosi hicho jana kwenda Musoma.

Advertisement

Kukosekana kwake kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Biashara United, huenda kukatoa nafasi kwa viungo wengine kama Erasto Nyoni au Mzamiru Yassin kuchukua nafasi yake, huku Onyango taarifa zinasema alikuwa akisikilizia maamuzi ya benchi lake la ufundi kama awepo safarini kwa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu wakianzia ugenini katika mechi dhidi ya Biashara na wikiendi hii kuvaana na Dodoma Jiji.

Hata hivyo, Daktari wa Simba, Yassin Gembe alipotafutwa ili kuelezea hali za wachezaji hao, alikiri Kanoute baada ya kupewa majibu yake kutoka hospitali anaendelea vizuri tofauti na awali alipougulia maumivu makali katika bega wakati akitolewa uwanjani na kupewa huduma ya kwanza uwanjani.

Dk. Gembe alisema kiungo huyo anaendelea na matibabu na hali yake ipo vizuri, huku Onyango mbali ya kupasuka usoni, lakini anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu na anaamini watapona haraka.

Advertisement