Kagera Sugar yaendeleza ubabe dabi ya Wakata miwa

TIMU ya Kagera Sugar imeendeleza makali yake kwenye mechi za Ligi Kuu baada ya leo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar na kuzidi kuendelea kuonyesha ubabe wao kwenye mechi za dabi ya Wakata miwa hao.

Bao pekee katika mchezo huo ambalo limeipa ushindi Kagera Sugar limefungwa na winga, Meshack Mwamita katika dakika ya 68 akipokea pasi ya Ally Ramadhan 'Kagawa' akamchungulia Kipa wa Mtibwa Sugar, Toba Kutisha na kufunga kwa mtindo wa 'kuchop'.

Ushindi huo ni wa tatu katika michezo mitano timu hizo zilipokutana kwenye Ligi misimu mitatu iliyopita, ambapo msimu uliopita (2021/2022) Kagera Sugar ilishinda mchezo mmoja na sare moja, msimu wa juzi (2020/2021) Kagera Sugar ilishinda moja na sare moja ambapo mara ya mwisho Mtibwa Sugar kupata ushindi katika dabi hiyo ni
Machi 7, 2020 iliposhinda mabao 3-1.

Mchezo wa leo ni wa 15 kwa timu hizo kukutana tangu mwaka 2015 ambapo Kahera Sugar imeshinda mara sita, Mtibwa Sugar mara saba na sare mbili huku Kagera ikifunga mabao 17 na Mtibwa akipachika 15 kukiwa hakuna kadi nyekundu kwenye mechi za dabi hiyo.

Ushindi wa leo ni wa pili mfululizo kwa Kagera Sugar katika Ligi baada ya kuichapa Tanzania Prisons mchezo uliopita huku ukiwa ni ushindi wa tatu kwa Kocha Mecky Maxime tangu aanze kuinoa kagera Sugar.

Mchezo wa leo ni wa tano kwa Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime tangu akabidhiwe mikoba ya Francis Baraza ambapo ameiongoza timu hiyo kwenye mechi tano za ligi akipoteza moja dhidi ya Yanga, akishinda tatu dhidi ya KMC, Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons huku akipata sare dhidi ya Mbeya City.

Bao ambalo amefunga Meshack Mwamita ni la pili kwake msimu huu na amefunga mfululizo mabao ambayo yameamua mechi na kuipa ushindi timu yake akifanya hivyo mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons timu yake ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini.

Kagera Sugar imecheza mechi 14 za Ligi ikishinda nne, sare tatu na kupoteza sita ikifunga mabao 13 na kuruhusu 15 ikivuna pointi 18 ikikamata nafasi ya tisa.

Mtibwa inasalia katika nafasi ya sita ikiwa na pointi 21 baada ya kucheza mechi 14 ikishinda sita, sare tatu na kupoteza tano huku ikifunga mabao 19 na kuruhusu 23.

Bao waliloruhusu leo Mtibwa Sugar linaifanya timu hiyo kuruhusu bao kwenye minne mfululizo ikipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Coastal Union na  Polisi Tanzania na kipigo cha 4-3 kutoka kwa Azam na 5-0 dhidi ya Simba.

Mchezo huo ambao umechezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanza saa 8 mchana umekuwa wa wazi kwa timu zote mbili ambazo zimeshambuliana kwa zamu huku Kagera Sugar ikitawala mchezo huo na kutengeneza nafasi nyingi.

Kipindi cha pili makocha wa timu zote mbili wamefanya mabadiliko ya wachezaji ambapo Kagera Sugar imewapumzisha Yusuph Mhilu, Meshack Mwamita, Anuary Jabir na Ally Ufudu na kuwaingiza Hamis Kiiza, Mbaraka Yusuph, Erick Mwijage na Yusuph Dunia katika dakika ya 46, 66, 73 na 88.

Kwa upande wake, Mtibwa Sugar imewapumzisha Adam Adam, Balama Mapinduzi, Ismail Mhesa, Nassoro Kiziwa na Onesmo Mayaya nafasi zao zikichukuliwa na Eliuter Mpepo, Omary Hassan, Omary Hamis, Ladaki Chasambi na Joseph Mkele katika dakika ya 63, 71 na 76.