Job akabidhiwa unahodha Yanga

Job akabidhiwa unahodha Yanga

KWA mara ya kwanza tangu ajiunge na Yanga msimu uliopita, beki Dickson Job leo atavaa kitambaa cha unahodha wakati chama lake likiikaribisha Mbeya Kwanza kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Job aliyewahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya vijana ‘Serengeti Boys’ mwaka 2017 na timu ya vijana ya Mtibwa Sugar sambamba na timu kubwa leo amepewa kitambaa hicho kutokana na nahodha mkuu, Bakari Mwamnyeto kuanzia benchi.

Akiwa kama kiongozi wa ndani ya uwanja leo, Job atacheza eneo la beki wa kati wa Yanga sambamba na Yannick Bangala huku Kibwana Shomari na Farid Mussa wakicheza beki za pembeni na Djigui Diarra akiwa golini.

Eneo la kiungo kwa Yanga leo wameanza Salum Abubakar ‘SureBoy’, Kharid Aucho na Said Ntibanzokiza ‘Saido’ huku eneo la ushambuliaji wakicheza Dickson Ambundo, Jesus Moloko na Fiston Mayele.

Aboutwalib Mshery, Mwamnyeto, Yassin Mustapha, Zawadi Mauya, Feisal Salum, Chico Ushindi, Crispin Ngushi, Denis Nkane na Herritier Makambo wataanzia benchi.

Yanga iliyo kileleni mwa msimamo na alama 60 ilizovuna kwenye mechi 24 inaingia kwenye mechi hii kutafuta pointi tatu zitakazoisogeza karibu na ubingwa kwa msimu huu.

Wakati huo huo Mbeya Kwanza iko mkiani na pointi 21 ikihitaji ushindi ili kujikwamua huko na kuepuka kushuka daraja zikiwa zimesalia mechi sita.