JICHO LA MWEWE: Miaka 21 baadaye, Simba katika mtego wa panya Cairo

ILICHUKUA dakika nne tu Simba kuruhusu bao ambalo hakuna aliyejua lingebakia kuwa la pekee la mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mechi nyingine tatu zilizobakia kwenda suluhu ya bila kufungana wikiendi iliyopita.

Ndio, haikushangaza sana. Imekuwa kawaida ya Simba kuruhusu mabao. Simba sio ngumu kufungika. Kama wiki chache tu zilizopita ilimruhusu Samson Mbangula kufunga mabao mawili pale Morogoro basi ingekuwa ngumu kuwazuia Al Ahly wasipate bao Temeke.

Ndicho kilichotokea. Sadio Kanoute alianza kukosa bao la wazi la mpira wa kona alipojikuta yuko peke yake, halafu upande wa pili Al Ahly walifanya kweli baada ya Percy Tau kumwacha Mohamed Hussein kisha akapiga krosi ambayo Henock Inonga aliiokoa vibaya, Ayoud Lakred akapambana, lakini mpira ukamrudia Ahmed Nabil Koka aliyefunga kwa urahisi.

Baada ya muda Simba wakauchukua mpira wao. Wakaumiliki. Sio jambo la kushangaza siku hizi. Al Ahly wanakuja uwanja wa taifa halafu wanahangaishwa.

Kuna watu watasema ni mpango mkakati. Ni kweli. Inawezekana wanacheza huku wakifikiria kumaliza mechi Cairo.

Hata hivyo, ninachopinga ni mpango mkakati wao haufanyiki kwa usahihi. Waliruhusu nafasi kwa Simba na zikapotezwa. Baada ya Kanoute kupoteza nafasi yake mapema kisha Saido Ntibazonkiza alipoteza nafasi yake. Willy Essomba Onana naye alipoteza nafasi yake.

Al Ahly hawakuifunga Simba kwa sababu ya uzoefu, hapana. Waliifunga Simba kwa sababu Wekundu hao hawakuwa na ubora katika eneo la umaliziaji. Waliwaruhusu Simba kupata nafasi kadhaa lakini Simba hawakuwa makini. Vinginevyo ingekuwa tunaongea hadithi nyingine.

Mpira hauhukumiwi na historia au ukubwa wa klabu. Unahukumiwa na dakika 90. Miaka michache nyuma Al Ahly pamoja na ukubwa wao walikwenda Pretoria kucheza na Mamelodi. Wakaruhusu nafasi kama hizi wakaadhibiwa 5-0. Nani mkubwa na ana uzoefu kati ya Al Ahly na Mamelodi?

Simba walipaswa kufanya hivi. Lakini haishangazi sana kuona hawakufanya hivi kwa sababu hata washambuliaji wao waliosajiliwa Januari kwa ajili ya kukitia makali kikosi hicho, Pa Jobe na Freddy Michael walikuwa wamekaa katika benchi wakitazama wenzao wakicheza.

Kocha Abdelhak Benchikha hakuwaamini. Viongozi hawawaamini. Mashabiki hawawaamini. Hakuna aliyeshangazwa kwa washambuliaji hawa wageni kukaa nje kwa sababu wamewatazama vizuri katika mechi chache za Ligi walizocheza.

Kisa? Ni mwendelezo ule ule wa kukosea kusajili. Unapowaondoa Moses Phiri na Jean Baleke huku ukimshutumu John Bocco kwa ‘kosa’ la kuzeeka basi unahitaji watu wa kweli sana kuweza kuifikia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati Simba wanapodai wanaitaka nusu fainali sijui huwa wanakuwa na ukweli wa moyoni kwa kiasi gani. Ukiitazama Simba ya sasa inayoitaka nusu fainali hauwezi kuilinganisha hata nusu na Simba ile ya kina Jose Luis Miquissone.

Ungeweza kuliona hilo pia katika kipindi cha pili cha pambano lenyewe. Simba waliishiwa nguvu. Waliishiwa kasi na pambano likawa la kawaida tu tofauti na dakika 25 za mwisho za kipindi cha kwanza. Wakati ule Simba walikuwa wanamaliza mpira kwa kasi na kufanya maajabu zaidi kipindi cha pili.

Sasa mwishoni mwa wiki hii, Simba watalazimika kuwa uwanjani kujaribu kumuenzi kwa vitendo beki wao wa kushoto wa kikosi cha mwaka 2003, Ramadhan Wasso ambaye alifariki dunia wiki iliyopita pale Bujumbura baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kwa nini? Wasso pamoja na Christopher Alex ndio wachezaji walioiaga dunia katika kikosi cha Simba ambacho kilisafiri mpaka Cairo kucheza na Zamalek na kisha kuwang’oa katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika huku wakiwa watetezi.

Ni kama ambavyo kikosi cha sasa kinalazimika kwenda hadi Cairo kuwang’oa Al Ahly katika ardhi ya nyumbani. Tofauti ya wakati ule na sasa ni wakati ule Simba waliwafunga Zamalek 1-0 pale Temeke halafu marudiano wakafungwa 1-0 na pambano likaenda katika penalti huku Simba wakifunga penalti zao zote na Zamalek wakakosa moja.

Safari hii wanalazimika kwenda Cairo na kufunga bao moja kisha kulilinda. Ni kazi ngumu, lakini ni lazima ifanyike. Tatizo tu ni Simba yenyewe inatia mashaka lakini ukweli ni wanacheza na Al Ahly ambayo hapana shaka ni ya kawaida sana katika macho yetu pengine kuliko wakati mwingine wowote ule.

Itakuwa kazi ngumu kucheza katika mazingira ya chuki kutoka kwa mashabiki wa Al Ahly. Hizi ni hatua ambazo wanabadilika zaidi, lakini Simba bado wana nafasi kama wakiweza kuchukua nafasi zao vema tofauti na walivyofanya Dar es salaam.

Haya yote yatakuwa yanafanyika, huku Al Ahly wakihitaji sare tu. sare yoyote. Hata hivyo siamini watacheza kwa ajili ya kusaka sare. Watacheza kwa ajili ya kusaka ushindi huku wakikumbuka namna ambavyo Simba waliweza kuwafungua na kutengeneza nafasi.

Bahati mbaya kwa Simba ni wakati huu wanakwenda Cairo kusaka ushindi. Kina Wasso walikwenda Cairo kwa ajili ya kusaka sare au kusaka wafungwe bao moja kisha waende matuta. Mpango wao ulifanikiwa.

Na sasa wanakwenda na Freddy kwa ajili ya kusaka ushindi. Itawezekana? Ni jambo la kusubiri na kuona lakini kwa hali ilivyo sasa kitu chochote kitachoifanya Simba isonge mbele kwenda nusu fainali inaweza kuwa maajabu kidogo. Kama wangekuwa wamefungwa Cairo, kisha marudiano ni Dar es Salaam lolote lingeweza kutokea lakini kwa hali ilivyo sasa wanapitia katika mstari wa kifo.