Inter yajitoa kwa Kante

MILAN ITALIA. INTER Milan imejitoa kwenye mpango wa kutaka kumsainisha kiungo wa Chelsea, N’Golo Kante kwa sababu Chelsea haihitaji kusikiliza ofa kwa ajili ya kumuuza mwamba huyo katika dirisha hili la usajili.

Kocha wa Inter, Antonio Conte ndio aliwasilisha pendekezo la Kante kusajiliwa kwa kuwa ni miongoni mwa wachezaji waliopigana kwa kiasi kikubwa mpaka yeye kuchukua ubingwa wakati anafundisha Chelsea mwaka 2017.

Hapo awali Chelsea iliripotiwa kukataa ofa ya Inter ambayo ilikuwa inahusu mabadilishano ya wachezaji ambapo Inter ilikuwa inataka kuwatoa Christian Eriksen na Marcelo Brozovic kama sehemu ya mabadilishano ili kumpata Kante.

“Kante ni mchezaji muhimu kwa Chelsea, sidhani kama itakuwa ni rahisi kwao kumuuza katika dirisha hili, tuna viungo nane ambao wanaweza kucheza nafasi yake hivyo tutajaribu kuwatumia hawa na kuhakikisha wanatupa matokeo,” alisema Piero Ausilio.

Kante amecheza mechi zote tatu za kwanza za Ligi Kuu na Chelsea inafikiria zaidi kumuuza Jorginho badala ya mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Ufaransa.

Ruben Loftus-Cheek na Ross Barkley pia ni miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kuondoka katika dirisha hili, Aston Villa na Southampton zimeonyesha nia ya kutaka kuwasainisha.

Ausilio pia alithibitisha klabu yake ilikuwa kwenye mazungumzo na Tottenham Hotspur ambayo ilikuwa inahitaji saini ya beki wao wa kati, Milan Skriniar lakini imeweka wazi kwamba haiwezi kuwauzia kwa kuwa Diego Godin pia anatarajia kuondoka.

Lakini ripoti nyingine zinaeleza Chelsea inaweza kumuuza Kante ili kupata pesa ya kumsajili Declan Rice kutoka West Ham.