Ihefu yaitibulia Yanga baada ya dakika 4,500

Hatimaye Yanga imemaliza rekodi yake ya kutopoteza katika michezo 49 baada ya leo kufungwa kwenye mchezo wao wa 50 dhidi ya Ihefu sawa na dakika 4,500 tangu walipopoteza mara ya mwisho.

Ihefu imemaliza rekodi hiyo ya Yanga baada ya kuwachapa vinara hao wa ligi kwa mabao 2-1 kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Real Estates Mbarali mkoani Mbeya.

Huo unakuwa ni ushindi wa tatu kwa Ihefu wakipanda mpaka nafasi ya 13 wakitoka mkia wa msimamo wa ligi, ambapo imeshinda mechi zote tatu wakiwa nyumbani msimu huu.

Katika mechi zote tatu walizoshinda Ihefu imetengeneza ushindi huo wakitumia mabao mawili ambapo wakianza kushinda dhidi ya Dodoma Jiji (2-0) kisha wakawachapa Coastal Union (2-1) na leo wakarudia matokeo kama hayo mbele ya mabingwa watetezi Yanga.

Mabao ya leo timu zote wameyatengeneza wakitumia mipira iliyokufa ambapo Yanga ambao wakiwa wa kwanza kupata bao  dakika ya 9 wakitumia mpira wa adhabu ndogo beki Yannick Bangala akifunga kwa kichwa mpira ukipigwa na beki mwenzake Joyce Lomalisa.

Wenyeji wakasawazisha kwa kupitia shambulizi kama hilo dakika ya 39 mpira ukipigwa na kiungo Mzimbabwe Never Tigere kabla ya beki Lenny Kissu kupiga bao la ushindi dakika ya 62 kwa mpira wa kona ya Tigere.

Hata hivyo licha ya Yanga kupoteza mchezo huo wa kwanza msimu huu wameendelea kusalia wakiongoza msimamo wa ligi wakisalia na pointi 32 baada ya michezo 13 huku wakiwa na mchezo mmoja pungufu dhidi ya Azam wanaowafuatia nafasi ya pili na Simba walioko nafasi ya tatu.

Pointi tatu za leo kwa timu hiyo imezishusha timu tatu za Dodoma Jiji, Polisi Tanzania na Ruvu Shooting na kukaa kwenye msitali wa njano kwa pointi 11 na kuipa nguvu na matumaini ya kukwepa rungu la kushuka daraja.

Ihefu inakuwa timu ya kwanza ligi kuu kuifunga Yanga ambayo kabla ya mchezo wa leo ilikuwa imecheza mechi 49 sawa na dakika 4,410 bila kupoteza na kuwatibulia wababe hao wanaotetea ubingwa wa ligi kuu kwa msimu wa pili mfululizo.

Timu hiyo ya mkoani Mbeya inaweka rekodi ya kwanza kuvuna ushindi kwenye uwanja wake Highland Estate dhidi ya Yanga na kuvunja uteja kwa vigogo hao ambao katika mechi tatu walizokuwa wamecheza awali, ilipoteza zote.

Pia inabaki kuwa miongoni mwa timu tatu hadi sasa, ambazo Straika wa Yanga na kinara wa mabao ligi kuu (10) Fiston Mayele ambazo hajafunga sambamba na Simba na Tanzania Prisons.

Yanga inakuwa mechi yake ya kwanza kufungwa kwenye ligi kuu katika misimu miwili mfululizo tangu Aprili 25, 2021 ilipopoteza dhidi ya Azam bao 1-0 likifungwa na Prince Dube uwanja wa Mkapa Dar es Salaam sawa na siku 582 na ikiwa kipigo cha tatu ikiwamo mechi mbili za klabu bingwa dhidi ya Rivers United, Septemba 12, 2021 wakilala 1-0 nyumbani kisha ugenini kufa tena 1-0 na Al Hilal walioshinda nyumbani 1-0 Oktoba 16 mwaka huu.

Bao la Yanick Bangala (Yanga) linakuwa la kwanza msimu huu, huku Never Tigere likiwa la pili akiifungia Ihefu huku Lenny Kisu naye akifunga bao lake la kwanza na kuipa ushindi muhimu timu yake na kuikwamua mkiani.