Ihefu SC mechi nane tu

MECHI nane zilizosalia katika lalasalama ya Ligi Kuu Bara ndiyo hesabu ya mwisho ya Kocha Mkuu wa Ihefu, Zuber Katwila kusalia ndani ya ligi hiyo msimu ujao.

Ihefu mpaka sasa inashikilia nafasi ya 18 baada ya kushinda michezo sita, sare sita na kupoteza michezo 14 wakiwa na pointi 24.

Katwila aliiambia Mwanaspoti jana kuwa, kwa sasa hesabu zake ni kuhakikisha anashinda michezo yote minane iliyosalia ili kujinasua katika hatari ya kushuka daraja.

Alisema kuwa ligi msimu huu imekuwa na ushindani mkubwa, huku kila timu ikipambana kuhakikisha inamaliza nafasi za juu na nyingine kama wao kutafuta nafasi ya kusalia katika ligi. “Naamini nafasi bado ninayo, napambana kwelikweli mechi zilizobakia nipate matokeo, hapo nitakuwa katika hatua nzuri ya kubaki kwenye ligi, ushindani ni mkubwa sana ila hatujakata tama,” alisema.

Katwila alisema kwa sasa wanaendelea na maandalizi ya mchezo wao na Tanzania Prisons utakaopigwa keshokutwa ambao utazidi kumpa mwanga wa hatima ya kikosi chake. Michezo ambayo Ihefu imesalia mpaka sasa ni dhidi ya Prisons, Coastal Union, Polisi Tanzania, Dodoma Jiji, JKT Tanzania, Kagera Sugar, Yanga pamoja na KMC.