Ibra Class atetea ubingwa GBC

Ibra Class atetea ubingwa GBC

Muktasari:

Bondia Ibrahim Class amefanikiwa kutetea ubingwa wa Dunia unaotmbuliwa na Chama cha GBC kwenye uzani wa Junior Lightweight, licha ya kupata upinzani mkali kutoka kwa mpinzani wake kutoka Zambia, Simon Ngoma.

Bondia Ibrahim Class amefanikiwa kutetea ubingwa wa Dunia unaotmbuliwa na Chama cha GBC kwenye uzani wa Junior Lightweight, licha ya kupata upinzani mkali kutoka kwa mpinzani wake kutoka Zambia, Simon Ngoma.
Class alitwaa ubingwa huo kwa ushindi wa majaji wote watatu,  95-91, 98-88 na 98-88 katika pambano kali na la kusisimua lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba.
Katika pambano hilo lilikuwa la piga nikupige, Class alipata upinzani mkali toka kwa Mzambia huyo aliyekuwa akipigana staili za ngumi ya mitaani zaidi ya kushambulia ovyo ovyo.
Mbali ya kusukuma, Ngoma alikuwa anapiga popote hata kisogoni na kusababisha mwamuzi wa pambano hilo, Pendo Njau kumuonya mara kwa mara na kufikia hatua ya kumkata pointi.
Class alionekana kuchanganyikiwa zaidi kutokana na staili ya Ngoma, naye alikutana na ngumi kali ya kulia na kuanguka chini katika raundi ya tatu ya pambano.
Kuona hivyo, Class alibadili staili ya kupigana na kuanza kumkwepa zaidi huku akipiga ngumi za kuvizia na kujikusanyia pointi nyingi sana.
Raundi ya nne ilikuwa ngumu kwa mabondia wote kwani kila mmoja alikuwa anashambulia na kupata pointi na kulifanya pambano hilo kuwa gumu kutabiri.
Class angeweza kushinda pambano hilo kwa knockout (KO) katika raundi ya nane, tisa na 10  kama sio kapeti la ulingoni kuteleza.
Ngoma ambaye alikuwa na kasi huku akitumia nguvu nyingi, safari hii ‘alipoa’ na hasa baada ya kupigwa ngumi nyingi sana kutoka kwa Class anayenolewa na kocha mzoefu, Habib “Master” Kinyogoli.
“Nimefurahi sana kutwaa mkanda wa dunia wa GBC, niliiutwaa nje ya nchi na kushindwa kuutetea kutokana na kukosa promota, namshukuru sana Mopao kwa kuandaa pambano la kuwania ubingwa,” alisema Class aliyedai alipanda ulingoni huku mama yake akiwa mgonjwa.
Tofauti na mabondia wengine, Ngoma hakupinga matokeo hayo na kusema atajipanga kwa ajili ya pambano linginela marudiano.
Katika mapambano mengine,  Abdallah Luwanja  alimshinda Hussein Ally Gobos kwa pointi wakati  bondia Kivu Abdi alishinda kwa pointi dhidi ya bondia mkongwe,  Maisha Samson na Haidari Mchanjo alimchapa kwa pointi Saidi Hussein. Pia Hamza Mchanjo alimchapa kwa pointi Juma Abdallah.