Huyu Barbara ni zaidi ya jembe

Tuesday February 23 2021
barbara pic
By Clezencia Tryphone

LEO ni siku ya 170 tangu klabu ya Simba ilipomwamini na kumpa nafasi Barbara Gonzalez kuwa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo.

Kama mmesahau, Barbara alitangazwa kuchukua nafasi ya Senzo Mazingisa aliyejiuzulu ghafla kabla ya kuibukia Jangwani akiwa Mshauri Mkuu wa klabu ya Yanga, Septemba 5 mwaka jana na ukipiga hesabu kwa siku zilivyokata tangu aanze kazi leo Februari 22 ni siku ya 170.

Ndani ya siku hizo mwanadada huyu wa shoka amefanya mambo makubwa kiasi cha kuwasisimua wengine hata wale waliokuwa wakimponda walipoteuliwa na kutangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji.

Barbara ni kama aliyeamua kuwajibu kwa vitendo wale wote waliombeza kwa mambo aliyoyafanya na Mwanaspoti limechambua mambo hayo kuthibitisha ni Mwanamke wa Shoka na ni zaidi ya jembe ndani ya klabu hiyo ya Msimbazi.


KUJENGA MSHIKAMANO

Advertisement

Barbara alianza majukumu yake ndani ya klabu kwa kujenga uhusiano mzuri kati ya wachezaji na viongozi kwa kuandaa semina mbalimbali.

Alipata nafasi ya kukaa na watendaji wote wa ndani na kubadilishana nao mawazo sambamba na wachezaji nao walipata nafasi hiyo.

barbara pic 1

Baada ya hapo Barbara alivuka mipaka ya Tanzania na kwenda kutengeneza uhusiano mzuri baina ya klabu yake na nyingine nje ya Nchi.

Ametembelea klabu kama Al Ahly, As Vita na nyinginezo akiwa na lengo la kuunganisha umoja na ushirikiano zaidi.

Septemba 21 Barbara alitembelea makao makuu ya klabu ya Al Ahly mchini Misri ikiwa ni safari yake kikazi aliyoambatana na Mjumbe wa Bodi Mulam Ng’ambi.

Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kujionea namna uendeshwaji wa klabu hiyo kubwa na yenye mafanikio barani Afrika na mikakati yao kiutendaji.

Barbara alikiri ziara hiyo ilimnufaisha sana, kwa kuwa alitambua na kujua mambo mengi na pia aliweza kujenga mahusiano ya kiutendaji baina ya klabu yake katika nyanja mbalimbali.

Mbali na Al Ahly pia alifanya ziara klabu ya Zamalek ambayo ni moja ya klabu kubwa yenye mafanikio ukanda huu wa Afrika.


SAFARI YAKE MISRI

Ndani ya muda mfupi aliokuwa nao mwanadada huyo ndani ya utendaji wake amefanikiwa kuteta na Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Ahmad Ahmad kwenye makao makuu ya shirikisho hilo yaliyopo jijini Cairo nchini Misri.

Septemba 24 mwaka jana, Barbara akiwa na Mulamu walipata nafasi ya kubadilishana mawazo na Rais huyo wa CAF na kumweleza namna ambavyo Simba ina mipango mikubwa.

Baada ya kukutana na Rais huyo alimpongeza kwa nafasi hiyo kubwa aliyoitwaa kama mwanamke akimtaka kuitumia vyema fursa hiyo ambayo itakuwa mfano kwa wanawake wengine.


UJIO WA SIMBA SUPER CUP

Unaweza kusema ni akili kubwa kwa mwanadada huyu asiyekuwa na mambo mengi, kwani baada ya klabu yake kutinga hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa akaona ni vyema timu ipate mechi nzuri za kimataifa zenye ushindani.

Barbara kwa kushirikiana na watendaji wenzake ndani ya klabu waliandaa kitu kinachoitwa Simba Super Cup ikiwa ni mashindano yaliyozikutanisha timu tatu ambazo ni TP Mazembe, Al Hilal na Simba.

Lengo la michuano hiyo ya tano ilikuwa ni kuipatia Simba mbinu na maarifa zaidi kutokana na timu ambazo zinashiriki michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Michuano hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam na Simba wakiwa wenyeji walitwaa ubingwa huo uliowafanya kujiamini zaidi.


MCHONGO WA KITALII

Mapema mwezi huu Simba itaanza kutupa karata yake katika michuano hiyo na Barbara aliwashangaza wengi baada ya kuingia ubia na Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza Nchi kupitia michuano hiyo.

barbara pic 2

Akili kubwa ya Barbara iliwazibua masikio wote waliokuwa wakimbeza juu ya utendaji wake katika nafasi hiyo kubwa na nyeti.

Simba iliingia makubaliano na wizara hiyo chini ya Waziri Dr Damas Ndumbaro kuitangaza kupitia jezi zao ambazo watazitumia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Simba katika jezi zao huwa na mdhamini Sportpesa lakini katika michuano hiyo hawawezi kutumia jezi zenye nembo hiyo kutokana na kanuni za CAF kutoruhusu kwani CAF wanamdhamini anayeshabiana na huyo wa Simba.

Hivyo, kuliko kwenda katika michuano hiyo kifuani pakiwa patupu, Barbara akaona kuna umuhimu wa kuweka kitu kikubwa ambacho ni faida kubwa kwa klabu na Taifa kwa jumla.

Wengi watajiuliza timu ambazo Simba inakutana nazo katika nchi hizo na utalii wapi na wapi jibu ni jepesi tu, wakati Simba wakiwa ndani ya dimba dakika 90 wataonekana katika runinga na mitandao mbalimbali ya kijamii hivyo itakuwa ni fursa kubwa zaidi.


REKODI YA DR CONGO

Barbara katika utendaji kazi wake wa muda mfupi ameweka historia ya Simba kwa kuwa timu ya kwanza kushinda katika ardhi ya Congo.

Simba imekuwa ikipata matokeo mabaya Congo ikikubali mara kwa mara vipigo vya mabao 5-0 lakini mwaka huu imekuwa tofauti.

Simba iliifunga As Vita bao 1-0 katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa, matokeo yaliyowashangaza wengi na mwanadada huyo akiweka rekodi ya kuingoza Simba kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kupata matokeo hayo.

Ushindi huo ulikuja baada ya kutoka kuandika rekodi nyingine ya kuiongoza Simba kupata ushindi nchini Nigeria ikiwa pia ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo na timu nyingine za Tanzania.


MSIKIE WAZIRI UMMY

Ukiwataja wanawake watatu bora hapa nchini hauwezi kuacha kumtaja Ummy Mwalimu mwanamama aliyeweza kuisimamia vilivyo Wizara ya Afya na changamoto zake zote na sasa anauonyesha utendaji wake katika wizara mpya ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

Ummy hajawa nyuma kufunguka namna anavyokoshwa na uwezo wa Barbara kama mwanamke katika nafasi kubwa anayoitumikia ndani ya Simba.

Ummy anasema, Barbara ajitahidi kuziba masikio pamba na kutoyasikiliza yasemwayo dhidi yake na kuonekana kumkatisha tamaa.

“Yatakuja maneno ya kumvunja moyo na kumkatisha tamaa, asiyasikilize azidi kusonga mbele namtakia mafanikio mema nina imani ataifikisha Simba mahali pazuri zaidi.”

“Barbara ni mmoja wa funzo kwa wanawake hasa vijana kuacha uoga na kujitosa katika nafasi mbalimbali zinapojitokeza, habari za kuogopa wanaume hakuna tunatofautiana jinsia tu na sio kiakili,” anasema Ummy.

Ummy anasema hapo awali hakumfahamu Barbara lakini utendaji wake mzuri unamfanya azidi kuonyesha kitu na kuwafundisha wanawake kuacha uoga na kupambania kile wanachokiamini.


MIPANGO YAKE

Licha ya kufanya vitu vikubwa ndani ya muda mchache na kuwafanya waliokuwa wakimbeza kunyoosha mikono juu, bado anasema kazi ndio kwanza ameanza.

Barbara anasema ana mipango mingi ambayo itakuwa na manufaa makubwa ndani ya klabu yao hivyo wanasimba wakae mkao wa kula na kuzidi kumuombea awe na afya njema.

Mwanaspoti lilikuwa gazeti la kwanza kufanya mahojiano na Barbara alipotangazwa katika nafasi hiyo na alieleza mipango yake mingi na inaonekana sasa.


TWFA WAFUNGUKA

Katibu wa Chama cha Soka cha Wanawake ( TWFA), Somoe Ng’itu anasema, uteuzi wa Barbara ndani ya Simba ni heshima tosha kwa wanawake kuwa wanaweza.

Somoe anasema, wanawake wanaweza na ndio maana Mtendaji huyo ameweza kuwaonyesha namna gani anayajua majukumu yake ya kwa muda mfupi waliokuwa wakimbeza amewajibu.

“Barbara ni mpambanaji, kama wadau wa soka la wanawake tunaipongeza Simba kama klabu kubwa kumpa nafasi nyeti mwanamke ambaye anaitendea haki vilivyo.”

Advertisement