Huko Liti, kuna matokeo ya kushtua, makocha waahidi boli matata

KWA matokeo ya mechi tano za Yanga ugenini sambamba na fomu ya mwisho ya Dodoma Jiji ikishinda bao 2-1 ugenini dhidi ya KMC, wadau wanatabiri matokeo ya kushtua leo kwenye mechi ya Yanga na Dodoma saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Liti Singida. Wenyeji Dodoma katika mechi zao nne za nyumbani wameshinda moja tu huku Yanga ugenini wakishinda zote tano lakini matokeo ya KMC yanawapa jeuri wenyeji wa kuja na sapraizi. Dodoma hawajawahi kushinda dhidi ya Yanga misimu miwili nyuma hivyo itakuwa inatafuta ushindi wake wa kwanza, ambao nao watakuwa wanafukuzia rekodi yao ya kutopoteza mechi 48.

Katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu, 2020/2021 Dodoma ilikuchapwa 3-1 Uwanja wa Benjamin Mkapa, marudiano, Dodoma ilijitutumua ikiwa nyumbani na kutoa suluhu lakini ikapoteza mechi nyingine mbili za msimu wa 2021/2022 ikianza kwa kuchapwa 4-0 na mechi ya marudiano Yanga ikashinda 2-0. Leo itakuwa mechi ya kwanza kwa msimu huu ambao kama wakishinda watakuwa wamevunja rekodi hiyo mbaya kwao.

Dodoma Jiji hadi sasa ipo nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo (15) ikiwa imecheza mechi 11, ikishinda mbili tu, kutoa sare tatu na kupoteza sita na alama tisa, namba ambazo haziibebi kitakwimu.

Kocha mkuu wa Dodoma Jiji, Melis Medo ambaye itakuwa mara yake ya kwanza kukutana na Yanga alisema mechi hiyo itakuwa ngumu lakini amewaanda vijana wake kupambana ili kupata matokeo mazuri.

“Kwa hali tuliyonayo kwa sasa tunahitaji zaidi ushindi kuliko matokeo mengine, kwa bahati mbaya tunaenda kucheza na Yanga timu ambayo ni ngumu na haijafungwa.” Mohammed Nabi wa Yanga alitamba kwamba watapambana uwanjani bila kutegemea historia na timu ipo kwenye morali nzuri.