Hizi hapa timu nne hazijafungwa na Mayele

FISTON Mayele gari limewaka. Mabao mawili aliyotupia dhidi ya Dodoma Jiji juzi, yamemfanya abakize timu nne tu ambazo hajazifunga kwenye Ligi Kuu Bara. Kila moja huko iliko inajiuliza ; “Sasa itakuwaje jamani.” Mayele anaongoza chati ya ufungaji bora Ligi Kuu msimu huu, lakini ametimiza mambo manne ambayo ni nadra kutokea katika ligi yetu.

Mayele alifikisha idadi ya mabao nane wakati huo akitimiza jumla ya mabao 24 aliyofunga katika Ligi Kuu Tanzania Bara ukijumlisha na 16 aliyopachika msimu uliopita.

Jambo la kwanza ni kubakiza timu nne ambazo hajazifunga katika ligi kati ya 15 nyingine ambazo ni Simba, Tanzania Prisons, Mbeya City na Ihefu huku zilizobakia nyingine 11 zikiwa zimeshawahi kuonja ladha ya kutunguliwa na Mayele ambaye mkewe amejifungua hivikaribuni.

Mabao yake mawili aliyopachika dhidi ya Dodoma Jiji juzi, yameufanya mguu wake wa kulia kuendelea kuwa wa dhahabu zaidi kwake kwani ndio amekuwa akiutumia kufungia idadi kubwa ya mabao kulinganisha na mguu wa kushoto na pia kichwa.

Kati ya mabao 24 aliyopachika Ligi Kuu, mabao 17 amefunga kwa mguu wake wa kulia huku moja tu akipachika kwa mguu wa kushoto na sita yaliyobakia akifumania kwa kichwa.

Jambo lingine la kushangaza kwa Mayele ni kuwa tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu Bara, yeye ndio mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika mechi za ugenini akifunga mabao 11 katika mechi tisa dhidi ya timu za Mtibwa Sugar, KMC, Mbeya City, Biashara United, Coastal Union, Azam FC, Polisi Tanzania, Dodoma Jiji na Geita Gold.

Mshambuliaji huyo amefungia mabao yake 24 katika viwanja tisa tofauti ambavyo ni CCM Kirumba, Sheikh Amri Abeid, Majimaji, Sokoine, Liti, Benjamin Mkapa, Azam Complex, Manungu Complex na Mkwakwani.

Mayele ni moto wa kuotea mbali zaidi katika kipindi cha kwanza kwani kati ya mabao 24 aliyofunga Ligi kuu, 15 amepata katika dakika 45 za mwanzo na mengine tisa amefunga kipindi cha pili.

Mshambuliaji huyo amefunga bao katika kila robo ya mchezo kati ya sita za dakika 90, na amekuwa hatari zaidi katika robo ya tatu ambayo ni dakika ya 31 hadi ya 45 ambapo katika muda huo amepachika mabao nane.

Kocha wa zamani wa Mbeya City na Tanzania Prisons, Adolf Rishard anasema kitu kikubwa kinachombeba Mayele ni kutokana na nyota huyo kujitambua na kufanya kazi yake kwa ufasaha tofauti na ilivyo kwa wengine. “Yuko siriazi na anachokifanya ndio maana tunaona anafanikiwa na kuisaidia timu yake kufanya vizuri hadi sasa, hii ndio maana ya mchezaji Profeshno lazima ajitofautishe na wengine.”

Kwa upande wa aliyekuwa Kocha wa Kagera Sugar, Mkenya Francis Baraza anasema Mayele ni mchezaji anayejieleza na kitu kikubwa anachofanikiwa kwa kiasi kikubwa nyota huyo ni kujituma na kuwa na uchu wa mafanikio.

“Anaonekana ni mchezaji aliyepata misingi bora ya mpira ndio maana anaimbwa kila kona, yupo hapa hivyo mpira lazima auwekee kipaumbele kwa kuwa ndiye ndugu yake wa kwanza,” anasema Baraza.

Naye Kocha Msaidizi wa Fountain Gate, Juma Masoud anasema anachokionyesha Mayele ni fundisho kubwa kwa wazawa kuongeza juhudi vinginevyo wataendelea kulalamika hawapewi nafasi kama wageni.

“Anajua kumalizia nafasi na hata mikimbio yake anapolielekea goli unaona kabisa amepevuka,” anasema Masoud.