Hata michezo mingine Zanzibar ilitisha pia!

KWA miaka mingi hadi miaka ya 1970 Zanzibar ilikuwa kitovu cha michezo katika Afrika ya Mashariki na Kati.

Hii ilitokana na visiwa hivi kuwa na watu wa makabila yote walioshiriki kila mchezo, tafauti na ilivyokuwa katika nchi za jirani na michezo kama ya gofu, kriketi, tenisi na mpira wa magongo ilionekana ni ya Wazungu na Wahindi.

Upo wakati baadhi ya vifaa vya michezo vilivyokuwa vya kisasa zama zile vilikuwa havipatikani kwa urahisi nchi jirani na kusababisha watu waliovihitaji kufika Zanzibar kuvinunua.

Karibu kila pembe ya miji na vijiji vya Unguja na Pemba kulikuwepo kiwanja cha michezo, lakini kwa bahati mbaya kukua kwa mahitaji ya majenzi kwa makazi, majengo ya ofisi, viwanda na biashara kumesababisha maeneo mengi kutoweka.

Hata uwanja wa wazi mkubwa kabisa Visiwani wa Mnazi Mmoja, mjini Unguja nao ulipunguzwa kwa karibu thuluthi moja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kisasa zilizopo Kikwajuni.

Uwanja wa gofu uliokuwa ndio mzuri kuliko yote Afrika Mashariki ulivamiwa na kujengwa nyumba.

Hii ilitokana na kasumba iliyotawala wakati ule, kriketi, gofu na tenisi ni michezo ya mamwinyi na mabwanyenye.

Mchezo wa ndondi nao ukapigwa marufuku kwa maelezo sio wa kiungwana kabla ya hivi karibuni sheria hiyo kuwekwa kando na miezi miwili iliopita mchezo huo ukaanza kufanyika Unguja.

Mara nyingi tangu miaka ya 1980, viongozi wa serikali wamekuwa wakieleza uamuzi wao wa kutaka kuimarisha michezo iliyokaribia kupotea visiwani ingawa kauli hizo hazikufuatiwa na vitendo.

Kwa karibu miaka 20 sasa kulikuwa na dalili za kuufufua mchezo wa kriketi na miaka sita iliyopita ilialikwa klabu maarufu ya kriketi ya Marleybone (MCC) ya Uingereza.

Klabu hii ilifanya  ziara Zanzibar 1957 pamoja na timu maaarufu za mchezo huo kutoka India na Pakistani.

Zanzibar ina historia ndefu ya mchezo wa kriketi ulioanza mwaka 1890 na tangu wakati ule hadi 1964, timu za Jeshi la Wanamaji la Uingereza zilifika Zanzibar mara kwa mara na kucheza na klabu za Visiwani, pia timu za India, akiacha zile za Tanganyika, Uganda na Kenya  zilitembelea Zanzbar

Zanzibar ilikuwa na klabu zaidi ya 10 za kriketi mpaka  yalipofanyika mapinduzi ya 1964. Hii ni mbali ya timu za shule za msingi na sekondari.

Wapo wachezaji walioweka  rekodi za aina yake na kuushangaza ulimwengu. Miongoni mwao ni Mzee Sherally aliyekuwa akiishi Darajani.

Siku moja alipiga mpira katika kiwanja cha Mnazi Mmoja na kuruka juu hadi kwenye mnara mdogo wa jumba la Makumbusho  lililopo pembezoni mwa barabara na kuvunja pambo la ndege wa chuma lililokuwa juu ya mnara mdogo.

Zanzibar pia ilitembelewa na timu maarufu na wachezaji wa michezo mbalimbali waliovuma wakati huo.

Miongoni mwa wachezaji maarufu waliofika Zanzibar ni mshambuliaji aliyetia fora duniani katika miaka ya 1950, Stanley Mathews wa Liverpool aliyekuja Zanzibar 1957 katika ziara yake ya Afrika iliyojumuisha nchi za Ghana na Afrika ya Kusini.

Alipokuja Zanzibar palikuwepo shamra shamra za aina yake na alipoondoka wachezaji vijana wengi walipewa jina la utani la kuitwa Stanley, kama tulivyoona wachezaji wa miaka ya karibuni kuitwa Pele, Maradona au majina ya wachezaji wengine maarufu duniani.

Stanley aling’ara mwishoni mwa miaka ya 1940 hadi 1965 alipojiunga na Stoke City akiwa na miaka 17. Baadaye aliichezea Potters na Blackpool na kuteremka uwanja wa Wembley akiwa na miaka 47 England ilipocheza na Brazil.

Mabaharia wa manowari na meli za Uingereza na India walikuwa na kawaida ya kufika Zanzibar baada ya kila miezi mitatu au mine na wakati wakiwepo Visiwani walicheza soka, mpira wa magongo au kriketi na timu za Zanzibar.

Mchezo wa ndondi ulipendwa sana na kulikuwepo mashindano kila mwisho wa mwezi na walikuwepo wapiganaji kama 12 ambao walikuwa wakichuana katika uzito mbalimbali.

Mmoja ambaye alikuwa ndio mbabe namba moja akiitwa Msafiri ambaye alikuwa anaishi Kikwajuni, karibu na Uwanja wa Mao Dzedung na alikuwa anasimamia klabu ya gofu hapo Uwanja wa Maisara.

Mzee huyu ambaye alisaidia sana kufundisha vijana wa Zanzibar mchezo huu pamoja na wana wa familia ya mzee Burgani Saaadat (aliwahi kuwa  waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) alipewa jina la utani la Msafiri Rocky ambalo ndio liliokuwa maarufu zaidi kuliko la baba yake.

Aliitwa Msafiri Rocky kwa vile masumbwi yake yalikuwa mazito kama mwanandondi wa Marekani, Rocky Marciano ambaye kuanzia nusu ya mwisho ya miaka ya 1940 hadi alipostaafu  1956 akiwa na miaka 31 hajawahi kushindwa pambanio hata moja.

Rocky Marciano kuna wakati alikuwa akifanya mazoezi kwa kupiga gogo la mti masumbwi na alishinda mara 49 mapambano ya uzito wa juu ya ndondi za kulipwa, 46 kwa ‘Knock Out’ na matatu kwa pointi.

Mingoni mwa mabondia  mashuhuri aliopambana nao ni  Joe Louis, Sonny Liston na Floyd Patterson.

Je, unajua Zanzibar kwenye ishu za sanaa na utamaduni nako kulinoga zaidi? Tukutane Jumatatu ijayo.