Gomes: Wakali wao ni wawili

Muktasari:

SIMBA inakwea Ijumaa na dege la kukodi kuelekea Botswana. Kocha mkuu, Didier Gomes amegundua kitu kwa mabeki wa pembeni wa timu hiyo ya Jwaneng Galaxy na watatumia nondo hizo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Jumapili hii.

SIMBA inakwea Ijumaa na dege la kukodi kuelekea Botswana. Kocha mkuu, Didier Gomes amegundua kitu kwa mabeki wa pembeni wa timu hiyo ya Jwaneng Galaxy na watatumia nondo hizo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Jumapili hii.

Gomes ameliambia Mwanaspoti kwamba yeye na timu yake wameshabaini kwamba timu hiyo ina ubora mkubwa wa kuchezea mpira na wanatumia mabeki wao wa pembeni kupeleka mashambulizi.

Ameiangalia timu hiyo kwenye mechi zake za raundi ya awali na yeye amejindaa kukabiliana nao ili kupata matokeo mazuri na tayari kambini amekuwa akiwafundisha wachezaji wake kwa namna mbalimbali ili kumaliza mechi hiyo ugenini.

“Wako vizuri kiukweli na wanajua sana kuuchezea mpira hilo tunatakiwa kujipanga nalo, mechi ni ngumu kwetu kama ya Platinums na hata ile timu zamani ya Luis (Miquissone) (Ud Songo) lakini sisi tunajiamini,” alisema.

“Inabidi tuwe na nidhamu na umakini mkubwa kwenye mchezo huu, ninaendelea kuzungumza na wachezaji wangu na kuwaambia umuhimu wa mechi hii, ngumu kufunga ugenini lakini ni muhimu kushinda ugenini,”alisema kocha huyo wa zamani wa El Merreikh ya Sudan.

Gomes pia alitamba kuwa na safu bora ya ulinzi ambayo inampa imani kubwa kuelekea katika mchezo huo baada ya beki wake Kennedy Juma kuonyesha uwezo mkubwa katika mechi ya Tanzania dhidi ya Benin.

“Kennedy amezidi kuwa bora kadri siku zinavyokwenda mbele, jambo zuri kuona anakomaa na kiwango chake kikipanda na ubora wake utafanya kuwe na upana wa kikosi changu kwa sababu nina Enock, Nyoni, Wawa na Onyango ambao wote ni wazuri,” alisema Gomes.


MUGALU

Gomes amempumzisha kiaina mshambuliaji wake Cris Mugalu na anamuandaa kwa ajili ya mchezo wa Jumapili.

Gomes alisema anamuamini mshambuliaji huyo atampa matokeo kutokana na ubora ambao anao anapokuwa uwanjani huku silaha kubwa ikiwa ni uwezo wa kupambana hata akiwa ameanza kucheza peke yake kama mshambuliaji.

“Alicheza na Dodoma alitoa pasi ya bao, aliumia kidogo baada ya mechi na alihitaji kupumzika na yupo kuangaliwa, atakuwa miongoni mwa wachezaji 18, namuhitaji kwenye kikosi changu.

“Ni mchezaji mzuri ambaye anaweza kucheza peke yake kama ilivyokuwa dhidi ya AS Vita na Al Ahly. Sawa amekosa mabao mengi dhidi ya Yanga lakini hauwezi kusema kama ni mchezaji mbaya,” alisema kocha huyo.