Gomes kumbe alirudi darasani mapema tu

BAADA ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kumtaja kocha  mkuu wa Simba, Didier Gomes kukosa sifa za kukaa benchi la ufundi la Simba kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa kutokana na kukosa sifa, uongozi wa timu hiyo umeibuka na kutolea ufafanuzi.

Gomes ana (UEFA A Diploma) na kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho hilo wanahitaji kocha awe na CAF A au UEFA PRO LICENCE.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu alisema ujio wa taarifa hiyo kwao si mpya kwani tayari kocha wao alishaanza kusoma.

"Hatujashtushwa na taarifa hizo kwani ni muda tu tulitaarifiwa na kocha akachukua maamuzi ya kusoma kwa njia ya mtandao (online) tunaimani hadi mchezo wetu unachezwa kocha atakuwa ameshamaliza masomo," anasema.

"Tunatarajia kucheza mechi yetu ya kwanza kati ya Oktoba 22 hadi 24 hivyo kulingana na hatua aliyoifikia tunaimani itaweza kuwa amekidhi vigezo hivyo atakuwa benchi kama kawaida," anasema.