Gomes apangua kikosi Simba ikiivaa Biashara

KOCHA mkuu wa Simba tayari ameweka wazi kikosi chake kitakachoanza mechi leo dhidi ya Biashara United kuanzia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Karume, Musoma.

Katika mchezo huo ambao Simba ipo ugenini, Gomes amemuanzisha kipa Aishi Manula ambaye ni kipa namba moja wa timu hiyo kwa muda mrefu.

Katika eneo la mabeki kuna mabadiliko matatu tofauti na ilivyozoeleka, Shomari Kapombe ameanza kama kawaida beki ya kulia huku kushoto akipangwa Israel Mwenda aliyesajiliwa kwenye Dirisha Kubwa la Usajili lililopita akitokea KMC.

Beki wa kati wamepangwa Kennedy Juma aliyekuepo msimu uliopita sambamba na Hennoc Inonga ‘Varane’ aliyesajiliwa kutokea DR Congo sambamba na Pascal
Wawa.

Erasto Nyoni na Rally Bwalya watacheza eneo la kiungo huku Meddie Kagere, John Bocco wakiongoza mashambulizi.

Kwa kikosi hicho, Kapombe na Israel watakuwa na kazi kubwa ya kupandisha mashambulizi kupitia pembeni huku Varane, Kennedy na Wawa wakicheza kama mabeki watatu wa nyuma.

Benchi wapo, Beno Kakolanya, Mohamed Hussein, Muziru Yassin, Pape Sakho, Peter Banda, Duncan Nyoni, Chriss Mugalu, Yusuph Mhilu na Jimmyson Mwanuke.