Gomes aanza na gia mpya, 8 waachwa Dar

KIKOSI cha Simba leo kitacheza mechi ya kwanza dhidi ya  Biashara United huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Didier Gomes akija kivingine akipiga hesabu za safari yao ya kutetea taji.

Gomes yupo na jeshi la watu 24, huku akiwaacha wachezaji nane jijini Dar ili kuhakikisha anashinda kesho na ile inayofuata dhidi ya Dodoma Jiji.

Walioachwa ni kipa Jeremia Kisubi, Ibrahim Ajibu, Abdulsamad Kassim, Gadiel Michael, Joash Onyango, Jonas Mkude, Sadio Kanoute na Ahmad Ferouz Teru watakuwa na programu maalumu chini ya Kocha wa viungo, Adel Zrane.

Sadio na Onyango wamebaki kwa vile ni majeruhi, huku Mkude akitoka katika matatizo ya kifamilia, Ajibu, Abdulasamad, Gadiel ikiwa ni sababu za kiufundi na kipa chipukizi Ahmed amerudishwa timu ya vijana.

Mratibu wa Simba, Abbas Suleiman alisema; “Wanaokwenda na kubaki ni la kocha mkuu, ila ujue tu wachezaji 24 watakuwa safarini nane watabaki Dar,” alisema.

Licha ya Mratibu huyo kutopenda kuzungumza kwa undani, lakini taarifa kutoka Simba zinasema kuwa, Kocha Gomes amepania kushinda mechi hizo za ugenini ili kutuliza machungu ya mashabiki wao baada ya kichapo cha Yanga cha bao 1-0.

Inaelezwa Gomes, hajafurahishwa na walivyocheza vijana wake, ila amekausha ili aelekeze akili katika Ligi Kuu ili watetee tena taji.

Simba imeifuata Biashara ikiwa na rekodi tamu dhidi yao, kwani tangu ipande haijawahi kushinda mbele ya Simba wala kupata sare.