Golini Yanga anakaa huyu, Metacha chali

ACHANA kwanza na beki wa kati Mkongomani, Henock Inonga ambaye yuko kwenye hatua za mwisho za kumalizana na Yanga ili atue nchini kujiandaa na kambi ya Morocco.

Yanga imeanza kushusha vifaa kimya kimya na sasa wamemshusha kipa mmoja hatari kutoka Burundi ambaye atakuwa langoni kwenye kikosi cha Kagame inayoanza wikiendi hii.

Lakini pia dili la Straika, Heritier Makambo limeiva muda wowote kufikia Jumatatu unaeza kuona picha la kushtua kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.

Kipa Yanga waliyemalizana nae ni Erick Johora ambaye ni Mbongo alikuwa anatumikia klabu ya Aigle Noir ambao ni mabingwa wa zamani wa Burundi anakotoka Saido Ntibazomkiza na Fiston Abdul Razak.

Hesabu za Yanga kumwinda Johora zinamuda mrefu ambapo baada ya kiwango bora alipokuja nchini mara ya mwisho kucheza dhidi ya Yanga katika mchezo wa wiki ya Mwananchi ndipo Mwanaspoti lilizinasa hesabu hizo za mabosi wa Yanga.

Johora ni raia wa Tanzania ambapo sasa ujio wake unaondoa nafasi ya Metacha Mnata kusaini mkataba mwingine ndani ya klabu hiyo baada ya awali kuzinguana na mashabiki na viongozi.

Ndani ya Yanga kuna mvutano wachahe wanataka Mnata apewe mkataba lakini watu wengi hawataki kipa huyo arejeshwe kufuatia kitendo chake cha kuwatusi mashabiki katika mchezo wake wa mwisho akiwa na jezi ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting.

Upande mwingine kipa aliyemaliza msimu na Yanga, Mkenya Farouk Shikhalo yupo njia panda huku vigogo wengi wakitaka apewe mkataba mpya kutokana na kiwango alichoonyesha haswa kwenye mechi za Simba chini ya usimamizi wa Kocha wa makipa Mkenya,Razack Siwa.

Changamoto kubwa ya hatma ya Shikhalo ni kwamba kocha wa timu hiyo Nesreddine Nabi amewataka mabosi wake kusubiri kidogo aangalie kama anaweza kupata kipa mwingine anakojua yeye.

Mabosi wa Yanga wamevutiwa na mabadiliko ya Shikhalo katika mechi ambazo amekaa golini hivi karibuni wakiona anazidi kubadilika lakini pia nidhamu yake ndani ya miaka miwili akiwa na Yanga.

“Unajua tunaona kwamba Shikhalo anazidi kuimarika inawezekana huyu kocha wake Siwa (Razack) amegundua wapi alikuwa anakosea unajua hawa wawili walifanya kazi pamoja.,” alisema mmoja wa viongozi wa usajili wa Yanga.

Shikhalo na Siwa walikuwa wakifanya kazi pamoja wakiwa Kenya na timu ya Bandari huku kipa huyo akiibuka kipa bora mara mbili mfululizo akiwa na timu hiyo.

Tayari Yanga imeshamjumuisha Johora katika kikosi chake cha Kombe la Kagame akiwa na makipa wengine wawili Ramadhan Kabwili na Geoffrey Magaigwa na kufanya sasa Yanga kuwa na jumla ya wachezaji 20 katika mashindano hayo.