Geita Gold, Singida Big Stars ngoma ngumu, sare zaendelea

DAKIKA 90 za chezo wa Ligi Kuu kati ya wenyeji Geita Gold na Singida Big Stars zimeshidwa kupata mbabe ambapo timu hizo zimetosha kwa kufungana bao 1-1.

Mchezo huo wa nne kwa timu zote umechezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambapo sare hiyo ni ya pili mfululizo kwa timu hizo na ya tatu kwa Geita Gold huku Singida Big Stars ikiendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo msimu huu.

Geita Gold ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tisa likifungwa na George Mpole akimalizia kiulaini pasi ya Dany Lyanga ambaye amemchambua kipa, Metacha Mnata. Bao hilo ni la kwanza kwa Mpole msimu huu baada ya kuambulia patupu katika mechi tatu za kwanza.

Singida ambayo imeuanza mchezo huo kwa kasi ya chini imepata bao la kusawazisha dakika ya 43 likifungwa na Rodrigo Fegu kwa shuti akimalizia kwa ufundi mpira mrefu wa Aziz Andambwile ambao umewababatiza mabeki na kumkuta nyota huyo.

Dakika 45 za kwanza zimemalizika timu hizo zikiwa nguvu sawa, ambapo  kipindi cha pili kimekuwa cha piga nikupige timu zote zikishambuliana kwa zamu lakini safu za ushambuliaji zimekosa umakini kutumia nafasi.

Dakika ya 64, Kelvin Sabatho amekosa bao la wazi baada ya kuwapita mabeki lakini shuti lake likatoka nje kidogo ya lango, mnamo dakika ya 69 nusura Rodrigo afunge bao la pili baada ya kuwachambua mabeki lakini shuti lake likawababatiza mabeki na kuokolewa.

Dakika ya 73, Rodrigo ameangushwa ndani ya eneo la penalti na beki Bakari Husseinambaye amemsukuma kwa mkono akiwa kwenye harakati za kufunga lakini refa akapeta huku benchi la ufundi la Singida na wachezaji wakidai penalti na kuibua kelele kwa mashabiki jukwaani wakimshangaa mwamuzi.

Dakika ya 76, Dario Frederico ameonyeshwa kadi ya njano baada ya kuupiga nje mpira kwa hasira wakati mwamuzi ameshapulizi filimbi, Seleman Ibrahim, Juma Mahadhi na Kelvin Yondani nap walionyeshwa kadi kama hiyo kwa nyakati tofauti.  

Dakika ya 77, Rodrigo ambaye leo ametakata nusura afunge kwa shuti la mguu wa kushoto lakini likaokolewa na kipa na kuwa kona isiyo na faida.

Timu zote zimefanya mabadiliko dakika 79, Geita ikiwatoa Saido Ntibanzokiza na Deusdedith Okoyo nafasi zao zikichukuliwa na Offen Chikola na Juma Mahadhi huku Singida ikimpumzisha Dario Frederico na kuingia Amissi Tambwe.

Mabadiliko mengine yamefanyika dakika ya 82, Singida ikimtoa Peterson Cruz na kuingia Miguel Escobar huku Geita ikimtoa Dany Lyanga na Adeyum Saleh na kuwaingiza Raymond Masota na Yahya Mbegu. Licha ya mabadiliko hayo milango ya timu zote imekuwa migumu kufunguka huku mabeki wakifanya kazi yao vyema, ambapo dakika 90 za mchezo huo zimemaliza kwa sare ya 1-1.

Kikosi cha Geita Gold: Sebusebu Samson, George Wawa, Adeyum Saleh, Bakari Hussein, Kelvin Yondani, Yusuph Kagoma, Suleman Ibrahim, Deusdedith Okoyo, George Mpole, Dany Lyanga na Saido Ntibazonkiza.

Singida Big Stars: Metacha Mnata,  Nicolas Gyan, Yasin Mustapha, Abdulmajid Mangalo, Paschal Wawa, Aziz Andambwile, Rodrigo Fegu, Bruno Gomes, Kelvin Sabato, Peterson Cruz na Dario Frederico.