Geay avunja rekodi ya taifa, afuzu Olimpiki

Muktasari:

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Geay kuchuana katika marathoni, akitokea kwenye mbio ndefu za uwanjani (mita 5,000 na 10,000) sanjari na nusu marathoni.

Mwanariadha Gabriel Geay wamevunja rekodi ya taifa ya marathoni na kufuzu kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki ya Julai nchini Japan.

Geay ameweka rekodi hiyo kwenye mbio za Generali milano marathoni zilizofanyika asubuhi ya leo Jumapili nchini Italia.

Katika mbio hizo, Mtanzania huyo alimaliza wa sita na kuandika rekodi mpya ya taifa ya marathoni lakini pia kufuzu kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki.

Mwanariadha huyo aliyetumia saa 02:04 kumaliza mbio hizo amevunja rekodi ya taifa ya saa 02:07 iliyowekwa na Augustino Sulle, Oktoba 2018 kwenye mbio za Toronto marathoni nchini Canada.

Muda wa saa 02:04 ni mkali zaidi kuandikwa kwenye mbio za marathoni nchini.

Awali rekodi ya taifa ilikuwa ikishikiliwa na Juma Ikangaa ya saa 02:08 aliyoiweka mwaka 1989 nchini Marekani, akivunja ile ya John Stephen Akhwari.

Akizungumzia rekodi hiyo, Geay ambaye ameshiriki marathoni ya kimataifa kwa mara ya kwanza alisema amekuwa na mwanzo mzuri kwenye mbio ndefu ya barabarani.

"Ndoto imetimia, sasa naelekeza nguvu kwenye Olimpiki," amesema Geay muda mfupi baada ya kumaliza mbio hiyo huku mwanariadha mwingine, Natalia Elisante ambaye pia amekimbia nchini Italia akishindwa kufikia viwango vya Olimpiki.

Geay sasa anaungana na wanariadha wengine, Alphonce Simbu na Failuna Abdi ambao tayari wamefuzu kushiriki Olimpiki.