Fei Toto aiwahi mapema Al Hilal

Muktasari:

  • Kambi ya Yanga imeshusha presha kutokana na urejeo wa kiungo wake tegemeo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyekuwa akisumbuliwa na majeraha ya nyama za paja.

Dar es Salaam. Kambi ya Yanga imeshusha presha kutokana na urejeo wa kiungo wake tegemeo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyekuwa akisumbuliwa na majeraha ya nyama za paja.

Fei Toto alipata majeraha hayo katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 17 ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-0.

Majeraha hayo yalimfanya mchezaji huyo kujiondoa katika kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki huko Libya dhidi ya wenyeji keshokutwa Jumanne na mwingine dhidi ya Uganda ‘The Cranes’ uliochezwa jana.

Meneja wa Yanga, Walter Harrison aliliambia Mwanaspoti kuwa Fei Toto atajiunga kikosi leo kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mechi zinazofuata za timu hiyo dhidi ya Ruvu Shooting na Al Hilal.

“Tunamshukuru Mungu kikosi kinaendelea vyema na mazoezi yake hapa Avic - Kigamboni na wachezaji wote ambao walikuwa majeruhi wapo fiti na wameungana na timu kwa ajili ya maandalizi ya mechi zilizo mbele yetu.

“Fiston Mayele na Khalid Aucho walipata majeraha madogo ambayo baada ya kupatiwa matibabu walishaungana na kikosi na mchezaji mwingine ambaye alikuwa majeruhi ni Feisal Salum ambaye naye ataanza mazoezi ya pamoja na wenzake kesho (leo) baada ya kupona majeraha yake ambayo yalimfanya ashindwe kusafiri na timu ya taifa,” alisema meneja huyo.

Harrison alisema kutokana na kundi kubwa la wachezaji kupata fursa ya kuitwa katika timu za taifa kwa ajili ya mechi za kimataifa za kirafiki, wamelazimika kujikita zaidi katika mazoezi ya kujenga stamina kwa wachezaji waliopo ingawa wanafanya pia yale ya mbinu.

“Tuna wachezaji kama 10 hivi wapo katika majukumu ya timu za taifa, hivyo tunalazimika kuendelea na mazoezi na hawa waliopo tukingoja waungane na wenzao japo muda uliopo hadi mechi zilizo mbele yetu ni mfupi.

“Kuhusu mechi za kirafiki tuko kwenye mpango wa kucheza moja kabla ya kukabiliana na Ruvu Shooting ambao hautakuwa wa wazi na timu ambayo tutaitangaza hapo baadaye,” aliongeza Harrison.

Yanga itakabiliana na Ruvu Shooting, Oktoba 3 katika mchezo wa raundi ya tano ya Ligi Kuu na siku nne baadaye itaikaribisha Al Hilal katika mchezo wa kwanza wa raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi zote zikichezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ushindi wa jumla katika mechi mechi mbili dhidi ya Al Hilal utaifanya Yanga itinge katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo haijahi kuingia tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 1998.

Yanga ilitinga katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 9-0 dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini katika raundi ya kwanza ikishinda kwa mabao 4-0 kwenye mechi ya kwanza na katika mechi ya marudiano ikipata ushindi wa mabao 5-0.

Na katika Ligi Kuu ya NBC, Yanga inaongoza msimamo ikiwa imekusanya jumla ya pointi 10 katika michezo minne iliyocheza dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union, Mtibwa Sugar na Azam FC.